Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

“Allaah akamkirimu kwa yale anayotaka na akamfunulia yale anayoyataka kumfunulia:

مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ

“Moyo haukukadhibisha yale aliyoyaona.”[1]

Bi maana Allaah maeneo hapo alimfunulia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kumfunulia. Allaah alimzungumzisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini hakumuona, kwa sababu Allaah haonekani duniani. Mtunzi amesema:

“Allaah amsifu na amsalimishe duniani na Aakhirah.”

Hii ni miongoni mwa haki zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); kumswalia na kumtakia amani wakati wa kutajwa kwake:

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Mtume. Hivyo enyi walioamini mswalieni na mumsalimu kwa salamu.”[2]

Kulipopambazuka asubuhi na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaeleza washirikina wa Makkah khabari hizi, ulizidi ukafiri wao na kumkadhibisha kwao. Wakaona kuwa hiyo ni fursa ya kumchafua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakasema:

“Sisi tunaenda Palestina kwa kutumia muda usiopungua mwezi mmoja ilihali yeye anasema kuwa ameenda ndani ya usiku mmoja.”

Baadhi ya wanyonge wa imani wakaritadi kwa sababu ya tukio hili. Kuhusu wale wenye imani ya kweli wakasimama imara na kusadikisha. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisafirishwa usiku kwenda msikiti wa al-Aqswaa watu wakaanza kuzungumziaaa jambo hilo. Wakaritadi watu waliokuwa wakimuamini na kumsadikisha. Wtu katika washirikina wakamwendea Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) na kusema: “Unasemaje kuhusu rafiki yako ambaye anadai kuwa amesafirishwa usiku kwenda Yerusalemu?” Akasema: “Amesema hivo?” Wakasema: “Ndio.” Akasema: “Kama amesema hivo basi amesema kweli.” Wakasema: “Hivi kweli unamsadikisha kuwa usiku ameenda Yerusalemu na akarejea kabla ya kupambazuka asubuhi?” Akasema: “Ndio. Mimi namsadikisha katika yaliyo mbali zaidi kuliko hayo; namsadikisha kuhusu khabari za mbinguni asubuhi au jioni.” Kwa ajili hiyo ndio maana akaitwa “Abu Bakr as-Swiddiyq”, msadikishaji.”[3]

Hii ndio imani imara na iliyokita mizizi ambayo haiyumbiyumbi.

[1] 53:11

[2] 33:56

[3] al-Haakim (3/62).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 90-91
  • Imechapishwa: 24/01/2023