81. Nasaha kwa wanawake wa leo wanaovaa sitara za kijanja

Kwa mujibu wa maoni haya ya Shaafi´iyyah inafaa kwa mwanamke leo hii kutoka nje hali ya kuwa amevaa nguo za kubana na zilizokamatana na mwili na kuonyesha maumbo yake kwa upambanuzi. Mavazi haya yanaweza kuwa yenye kuonyesha maumbo kiasi cha kwamba hata ambaye yuko mbali akafikiri kuwa yuko uchi. Mfano ni kama hizi suruwali za soksi zinazoonyesha umbo la miguu na mapaja na kuyapmba zaidi, bali hata kaptupa ambayo inaonyesha maumbile ya paja. Kwa mtazamo wao zinafaa ikiwa mwanamke atavaa mavazi kama hayo, kwa sababu zimefunika ile rangi ya ngozi hata kama soksi hizo zitamfanya mwanamke kuonekana na rangi nzuri zaidi kuliko ile rangi yake ya asili. Hivi kweli kuna muislamu awezaye kusema kuwa haya yanafaa? Hili peke yake ni miongoni mwa dalili nyingi juu ya ulazima wa kujitahidi na kutofuata kichwa mchunga.

Kwa mnasaba huu napenda kutumia fursa ya kusema kwamba wasichana wengi waumini wanachojali ni kufunika kichwa na kifua peke yake na sambamba na hilo wanavaa mavazi ya kubana na mafupi ambayo hayazidi nusu ya mguu. Au yanafunika nusu ya chini ya mwili wa chini kwa suruwali za soksi ambayo zinamzidishia uzuri. Pengine baadhi yao wakaswali katika muonekano huu. Ni wajibu kwao kuhakikisha wanakamilisha kujifunika kama alivyoamrisha Allaah (Ta´ala), na kwa ajili ya kuwaigiliza Maswahabah wa kike ambao walirarua blanketi zao ili kujifunika kwazo wakati Allaah alipoamrisha kujiteremshia shungi. Hata hivyo sisi hatuwataki kupasua kitu katika nguo zao, isipokuwa tu wavae mavazi marefu na yenye kupwaya ili liwe ni vazi linalofunika yale yote ambayo Allaah ameamrisha kuyafunika. Nimewaona wengi katika wasichana waliodanganyika na baadhi ya wale wanaodaiwa kuwa ni katika walinganizi wa kike. Wamefanya ni alama kwao kufupisha kanzu zao hadi nusu ya mguu na soksi zinazoonyesha maumbo ya miundi. Ukiongezea ya kwamba wanavaa kichwani shungi peke yake pasi na kuweka jilbaab juu ya shungi hizo, kama ilivyoamrishwa ndani ya Qur-aan. Wanawake hawa hawafahamu kuwa wanaingia ndani ya wale ambao Allaah amesema juu yao:

الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا

”Wale ambao wamepoteza juhudi zao katika uhai wa dunia nao wakidhani kwamba wanatenda vizuri.”[1]

Nawanasihi wale wanawake wakweli miongoni mwao wasitangulizi mbele ya Qur-aan na Sunnah kipote au Shaykh wa kiume, sembuse Shaykh wa kike yeyote. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلَا تَتَّبِعُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۗ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ

“Fuateni yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu na wala msifuate badala Yake wasaidizi wengine. Ni machache mnayoyakumbuka.”’[2]

[1] 18:104

[2] 7:3

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 133-134
  • Imechapishwa: 16/10/2023