80. Vazi la mwanamke la kuswalia na la kutokea

Shaafi´iyyah wameleta maoni ya ajabu pale waliposema:

”Ama ikiwa nguo inafunika ngozi ya mwili na kuonyesha maumbo ya viungo haina neno. Kwa mfano suruwali ya kubana.”

Wanasema:

”Inapendeza mwanamke kuswali akiwa na kanzu iliyopwaya, shungi na avae jilbaab nene ili yasionekane maumbo yake.”[1]

Kusema kuwa inapendeza peke yake inapingana na uwajibu kama ilivyotangulia. Maneno ya Imaam ash-Shaafi´iy yanayokuja mbele yanafanana na niliyoyasema. Amesema:

”Akiswali na nguo yenye kuonyesha mwili swalah yake haitosihi… Naona kuwa inachukiza akiswali ndani ya nguo moja inayoonyesha maumbo ingawa haionyeshi kwa ndani. Aidha ni kana kwamba hatolazimika kuirudi swalah yake. Hali ya mwanamke ni yenye khatari zaidi akiswali na mtandio na kanzu vinavyoonyesha maumbo. Napendelea zaidi asiswali isipokuwa ndani ya jilbaab juu yake ili kanzu hiyo isiyonyeshe maumbo ya mwili.”[2]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

”Ni lazima kwa mwanamke kuswali ndani ya nguo tatu: kanzu, jilbaab na shungi.” ´Aiashah mwenyewe alikuwa akifunga kiunoni shuka yake ya chini na akiitumia kama jilbaab.[3]

Alikuwa akiswali hivo ili jilbaab hiyo isiyonyeshe kitu katika maumbo yake ya mwili. Maneno yake aliposema ”ni lazima” yanajulisha ya kwamba ni wajibu. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema maneno yenye maana kama hiyo:

”Anaposwali mwanamke basi aswali ndani ya nguo zake zote: kanzu, shungi na jilbaab.”[4]

Haya yanazidi kutilia nguvu yale tuliyotangulia kusema, kwamba ni wajibu kwa mwanamke kuvaa shungi na jilbaab vyote viwili pale anapotoka nje ya nyumba.

[1] Yamesemwa na ar-Raafi´iy katika tafsiri yake (4/92) na (4/105) pamoja na ”Sharh-ul-Muhadhdhab”.

[2] al-Umm (1/78).

[3] Ibn Sa´d (8/71)  kwa cheni ya wapokezi yenye sharti za Muslim.

[4] Ibn Abiy Shaybah (1/26/2) kwa cheni ya wapokezi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 133-135
  • Imechapishwa: 16/10/2023