Kuapa ni kula yamini. Maana yake ni kutilia nguvu hukumu kwa kumtaja muadhimishwaji kwa njia maalum. Kuadhimishwa ni haki ya Allaah (Ta´ala). Kwa hivyo haijuzu kuapa kwa asiyekuwa Allaah. Wanachuoni wameafikiana juu ya kwamba haifai kuapa kwa asiyekuwa Allaah na majina na sifa Zake. Vilevile wameafikiana juu ya makatazo ya kuapa kwa mwengine asiyekuwa Yeye[1]. Kuapa kwa mwengine asiyekuwa Allaah ni shirki. Hayo ni kutokana na yale aliyopokea Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuapa kwa asiyekuwa Allaah amekufuru au ameshirikisha.”[2]

 Ni shirki ndogo. Isipokuwa ikiwa yule muapaji anamuadhimisha yule anayemuapia katika kiwango cha kumwabudu. Hapo itakuwa shirki kubwa, kama ilivyo hali kwa waabudia makaburi. Huwaogopa wale wanaowaapia katika watu wa makaburi zaidi kuliko wanavyomwogopa na kumuadhimisha Allaah kwa njia ya kwamba anapoambiwa mmoja wao kuapa kwa walii anayemuadhimisha hathubutu kufanya hivo akiwa si mkweli. Na anapoambiwa kuapa kwa Allaah, basi huthubutu kufanya hivo japo si mkweli.

Kuapa kwa njia ya kumtukuza kiumbe ni jambo lisilostahiki isipokuwa tu kwa Allaah. Ni lazima watu kuheshimu viapo. Watu wasiapeape sana. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ

“Na wala usimtii kila mwingi wa kuapa, anayedharauliwa.”[3]

وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ

”Chungeni yamini zenu.”[4]

Bi maana msiape isipokuwa wakati wa haja na katika hali ya ukweli na wema. Kwa sababu kuapa kwa wingi au kutumia uongo katika kiapo ni mambo yanayofahamisha kuwa mtu anamdharau Allaah na hamtukuzi, mambo ambayo yanapingana na ukamilifu wa Tawhiyd. Imepokelewa katika Hadiyth kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu aina tatu Allaah hatowasemeza, hatowatukuza na watakuwa na adhabu iumizayo.” Akatajwa mmoja wao: “Mtu ambaye amemfanya Allaah kuwa bidhaa yake; hanunui isipokuwa kwa kumuapia, hauzi isipokuwa kwa kumuapia.”[5]

Kuna matishio makali juu ya kuapa-apa kwa wingi katika mambo yanayofahamisha uharamu wake kwa sababu ya kuliheshimisha jina la Allaah na kumtukuza (Subhaanah). Vivyo hivyo ni haramu kuapa kwa Allaah kwa kusema uongo. Hicho ndicho kiapo cha uongo. Allaah amewasifu wanafiki kwamba wanaapa kwa kusema uongo na huku wanajua. Yanafupishwa hayo ifuatavyo:

1- Uharamu wa kuapa kwa asiyekuwa Allaah (Ta´ala). Kama kuapa kwa amana, kwa Ka´bah au Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba hiyo ni shirki.

2- Uharamu wa mtu kukusudia kuapa kwa jina la Allaah kwa kusema uongo.

3- Uharamu wa kuapa-apa kwa wingi kwa jina la Allaah – ijapokuwa ni mkweli – ikiwa mtu hakuhitajia kufanya hivo. Kwa sababu huko ni kumdharua Allaah (Subhaanah).

4- Kufaa kuapa kwa Allaah mtu akiwa ni mkweli na ikiwa ni kwa haja.

[1] Maelezo ya chini ya ”Kitaab-ut-Tawhiyd”, uk. 303 cha Ibn Qaasim.

[2] Ahmad (6072), Abu Daawuud (3251) na at-Tirmidhiy (1539).

[3] 68:10

[4] 08:89

[5] at-Twabaraaniy (6111). al-Haythamiy amesema katika ”Majma´-uz-Zawaaid” (04/78):

“Wanaume wake ni wanaume Swahiyh.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 141-142
  • Imechapishwa: 09/06/2020