Hirizi ni ile inayovishwa shingoni mwa mtoto ili kumlinda na kijicho. Hirizi hiyohiyo anaweza kuvishwa nayo mtu mwanamume au mwanamke. Imegawanyika sampuli mbili:

Aina ya kwanza ya hirizi: Hirizi ya Qur-aan. Hirizi hiyo inaandikwa Aayah ya Qur-aan au majina na sifa za Allaah na akaivaa ili ajiponye kwayo. Wanachuoni wametofautiana katika maoni mawili juu ya hukumu ya kuivaa:

1- Maoni ya kwanza yanasema kuwa inafaa. Haya ni maoni ya ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw. Vilevile ndio dhahiri ya yale yaliyopokelewa kutoka kwa ´Aaishah. Maoni hayo ndio ya Abu Bakr al-Baaqir na Ahmad bin Hanbal katika moja ya mapokezi yake. Hadiyth inayokataza kuvaa hirizi wameifasiri kwamba inahusiana na zile hirizi zilizo ndani yake na shirki.

2- Maoni ya pili wanakataza jambo hilo. Hayo ni maoni ya Ibn Mas´uud na Ibn ´Abbaas. Ndio dhahiri ya maoni ya Hudhayfah, ´Uqbah bin ´Aamir na Ibn ´Akiym. Kuna kikosi cha Taabi´uun wenye kuonelea hivo wakiwemo wanafunzi wa Ibn Mas´uud, Ahmad katika moja ya mapokezi yake na ndio maoni yaliyochaguliwa na wanafunzi zake wengi na wakayachukulia kwa njia ya kukata wale waliokuja nyuma na wakatumia hoja kwa yale aliyopokea Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia: “Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakika ya matabano, hirizi na at-Tiwalah ni shirki.”[1]

at-Tiwalah ni kitu kinachotengenezwa wanachodai kwamba kinamfanya mwanamke kupendwa na mume wake na mwanamme na mke wake.

Maoni haya ya pili ndio sahihi kwa sababu tatu:

Ya kwanza: Ueneaji wa makatazo na hakuna kinachokhusisha ule ueneaji.

Ya pili: Kufunga njia zote. Kwani itapelekea kutundika na kuvaa yasiyofaa.

Ya tatu: Akivaa kitu katika Qur-aan basi yule mvaaji anaweza kupewa mtihani wa kuivaa katika hali ya kukidhi haja, kujisafisha kutokamana na haja na mfano wa hayo[2].

Aina ya pili ya hirizi: Zile hirizi wanazovaa watu ambazo si za Qur-aan kama shanga, mifupa, shell, nyuzi, viatu [vya wanyama], misumari, majina ya mashaytwaan na majini na talasimu. Hii ni haramu kwa kukata kabisa. Isitoshe ni shirki. Kwa sababu ni kumtegemea asiyekuwa Allaah (Subhaanah), majina, sifa na Aayah Zake. Imepokelewa katika Hadiyth:

“Atakayevaa/atakayejifungamanisha na kitu basi huwakilishwa kwacho.”[3]

Bi maana Allaah atamuwakilisha kwa kitu hicho alichokivaa au kujifungamanisha nacho.

Kwa hivyo yule mwenye kumtegemea Allaah, akamwelekea na akamwegemezea mambo yake yote Kwake basi humtosheleza, humkaribishia kila kilichokuwa mbali na humwepesishia kila gumu. Na yule mwenye kuwategemea wengine katika viumbe, akategemea hirizi, madawa na makaburi basi Allaah atamwakilisha katika mambo hayo ambayo hayatomtosheleza kutokamana na kitu, hayamiliki juu yake madhara wala manufaa. Hivyo ´Aqiydah inakhasirika na mafungamano yake na Mola Wake hukatika na Allaah anamdhalilisha.

Ni wajibu kwa muislamu kuichunga ´Aqiydah yake kutokamana na yale mambo yanayoiharibu au kuitia kasoro. Asifanye tiba zisizojuzu, asiende kwa makhurafi na waganga kujitibisha maradhi alionayo. Watu hao watamgonjwesha moyo na ´Aqiydah yake. Mwenye kumtegemea Allaah humtosheleza.

Baadhi ya watu huvaa vitu hivi miilini mwao ilihali hawana maradhi yenye kuhisiwa. Bali ana maradhi ya kufikiria ambayo ni kuogopa kijicho na hasadi. Wakati mwingine wanavitundika juu ya gari yake, mnyama wake, mlango wa nyumba yake au wa dukani mwake. Yote haya ni kutokana na ´Aqiydah dhaifu na udhaifu wa kumtegemea kwake Allaah. Hakika udhaifu wa ´Aqiydah ni maradhi ya kihakika ambayo yanatakikani kutibiwa kwa kuijua Tawhiyd na ´Aqiydah sahihi.

[1] Ahmad (3615), Abu Daawuud (3883) na Ibn Maajah (3530).

[2] Fath-ul-Majiyd, uk. 136.

[3] Ahmad (18803) na at-Tirmidhiy (2077).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 138-140
  • Imechapishwa: 09/06/2020