Matabano ni ulinzi anasomewa yule mwenye maradhi kama homa, kifafa na maradhi mengineyo. Huitwa pia “´Azaaim”. Yemegawanyika aina mbili:

Ya kwanza: Ambayo imesalimika kutokamana na shirki. Aina hii ni ile ambayo mgonjwa akasomewa kitu kutoka katika Qur-aan au akalindwa kwa majina na sifa za Allaah. Aina hii inafaa. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya matabano, akaamrisha matabano na akayajuzisha. ´Awn bin Maalik amesimulia kwa kusema:

“Tulikuwa tukifanya matabano wakati wa kipindi kabla ya kuja Uislamu tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Unaonaje juu ya hilo?” Akasema: “Nionyesheni matabano yenu. Matabano hayana neno muda wa kuwa sio shirki.”[1]

 as-Suyuutwiy amesema:

“Wanachuoni wameafikiana juu ya kujuzu kwa matabano ikikusanya sharti tatu:

1- Iwe kwa maneno ya Allaah au kwa majina ya Allaah na sifa Zake.

2- Iwe kwa lugha ya kiarabu na yale yanayojulikana maana yake.

3- Mtu aamini kuwa matamano hayaathiri kwa dhati yake, bali kwa makadirio ya Allaah (Ta´ala).”[2]

Namna yake ni mtu anasoma na kupuliza cheche za mate kwa mgonjwa au akasoma ndani ya maji na akammwagia mgonjwa, kama ilivyokuja katika Hadiyth ya Thaabit bin Qays:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichukua mchanga kutoka Butwhaan, kisha akauweka ndani ya chombo, kisha akaweka maji na kusoma na akammwagia nayo.”[3]

Ya pili: Ambayo hayakusalimika kutokamana na shirki. Hayo ni yale matabano ambayo anatakwa msaada mwengine asiyekuwa Allaah katika kumuomba du´aa, kuombwa uokozi na kuombwa ulinzi mwengine asiyekuwa Allaah. Kama mfano wa kufanya matabano kwa majina ya majini, majina ya Malaika, Mitume na waja wema. Huku ni kumuomba du´aa mwengine asiyekuwa Allaah, jambo ambalo ni shirki kubwa. Au inakuwa kwa lugha nyingine isiyokuwa ya kiarabu au mambo yasiyojulikana maana yake. Kwa sababu kunachelea kusiingie ndani yake shirki au kufuru pasi na mtu kujua. Aina hii ya matabano ni yenye kukatazwa.

[1] Muslim (5696).

[2] Fath-ul-Majiyd, uk. 135.

[3] Abu Daawuud (3885).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 137-138
  • Imechapishwa: 09/06/2020