71. Dalili kwamba kumtaka ulinzi Allaah ni ´ibaadah II

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

                      قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ

”Sema: “Najikinga na Mola wa watu.”[1]

MAELEZO

 Maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ

”Sema: “Najikinga na Mola wa watu.”

Allaah (´Azza wa Jall) ameamrisha kutaka ulinzi kwa Mola wa watu, mfalme wa watu na mungu wa watu. Yote haya ni majina na sifa za Allaah (´Azza wa Jall). Ndani yake kuna aina tatu za Tawhiyd; Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat.

Ameomba ulinzi kwa Allaah na kwa majina na sifa hizi. Ametaka ulinzi kutokamana na shari za yule anayetia wasiwasi ambaye ni shaytwaan. Shaytwaan humtia wasiwasi mtu, kumfanya akafikiria mambo na akamshughulisha ili atie ndani ya moyo wake mashaka, usitaji na kuchanganyikiwa katika mambo yake na khaswa katika mambo ya ´ibaadah. Hakika shaytwaan anamtia wasiwasi mtu katika ´ibaadah mpaka amtatize swalah na ´ibaadah zake. Hatimaye mambo yanaishilia kwamba anatoka nje ya swalah yake na anaamini kuwa imebatilika. Wakati mwingine mtu anaweza kuswali kisha akaamini kuwa hana wudhuu´, hakusimama kwa ajili ya kitu fulani au kwamba hakufanya kitu fulani. Matokeo yake anakuwa ni mwenye wasiwasi na hana utulivu katika ´ibaadah zake. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ametupa dawa ya khatari hii na hivyo ni kwa kuomba ulinzi kwa Allaah kutokamana na shari ya wasiwasi huu.

Khannas ni yule anayebaki nyuma na kujiweka mbali. Anatia wasiwasi pindi watu wanapoghafilika kumtaja Allaah na anajitenga mbali pindi watu wanapomtaja Allaah (´Azza wa Jall). Ni mwenye kutia wasiwasi pamoja na upumbaaji na ni mwenye kujitenga mbali wakati wa kumtaja Allaah (´Azza wa Jall).

الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ

“Anayetia wasiwasi nyoyoni mwa watu miongoni mwa majini na watu.”

Ni kana kwamba maana ni – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – kwamba wako wenye kutia wasiwasi katika majini na watu ambao wanawatia watu wasiwasi ambao wanawajia watu na kuwatia wasiwasi. Kama ambavo majini wana mashaytwaan wanaotia wasiwasi basi vivyo hivyo watu wana mashaytwaan wanaotia wasiwasi. Kwa hiyo wewe unamwomba Allaah ulinzi kutokamana na shari ya makabila haya mawili. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakujilinda mwenye kujilinda kwa mfano wa hizo mbili.”[2]

Bi maana kwa Suurah mbili hizi.

Kwa hiyo muislamu anatakiwa kuzisoma baada ya kila swalah, azikariri na azisome pia wakati wa kutaka kulala pamoja na Aayat-ul-Kursiy na Suurah “al-Ikhlaasw”. Anatakiwa asome Aayat-ul-Kursiy, Suurah “al-Ikhlaasw”, “al-Falaq” na “an-Naas”. Azisome baada ya kila swalah, azikariri mara tatu baada ya Maghrib na baada ya Fajr. Kadhalika azisome wakati wa kutaka kulala ili shaytwaan ajiweke naye mbali, asimuweze na asimsumbue usingizini mwake na akamshtua kwa ndoto mbaya.

Kinacholengwa kwa Suurah mbili hizi ni kwamba Allaah ameamrisha kuomba ulinzi Kwake pekee. Ni dalili yenye kufahamisha kwamba kumuomba ulinzi mwengine katika majini, watu au viumbe wengine haifai. Kwa sababu ni aina moja wapo ya ´ibaadah.

[1] 114:01

[2] Abu Daawuud (1463), an-Nasaa´iy (08/253) na Ahmad (28/530) (17297).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 149-151
  • Imechapishwa: 30/12/2020