70. Dalili kwamba kumtaka ulinzi Allaah ni ´ibaadah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kutaka kinga ni Kauli Yake (Ta´ala):

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ

”Sema: “Najikinga na Mola wa mapambazuko.”[1]

MAELEZO

Kuomba ulinzi ni kutafuta kimbilio kwa ambaye anaweza kukulinda kutokamana na chenye kudhuru unachokiogopa ili aweze kukulinda kutokamana na kitu hicho. Huku ndio kuomba ulinzi.

Kuomba kinga ni aina moja wapo ya ´ibaadah. Kwa msemo mwingine haijuzu kutaka ulinzi kwa asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hiyo yule mwenye kutaka ulinzi kwa kaburi, sanamu au yenginevyo asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall) basi ameshirikisha shirki kubwa. Amesema (Ta´ala):

وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا

”Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa watu wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia mzigo.”[2]

Waarabu, kipindi chao kabla ya kuja Uislamu, ilikuwa wanapotua maeneo fulani basi mmoja wao anasema:

“Najilinda na bwana wa bonde hili.”

Akikusudia mkuu wa majini. Kwa hiyo anamwomba ulinzi kutokamana na shari ya wafuasi wake wapumbavu. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema akiwa ni mwenye kubatilisha jambo hilo na hali ya kubainisha yale yaliyowekwa katika Shari´ah:

“Yule atakayeshuka nyumba fulani akasema:

أعوذ بكلمات الله التامات من شر ما خلق

“Najilinda kwa maneno ya Allaah timilifu kutokamana na shari ya alivyoviumba.”[3]

basi hatodhuriwa na kitu mpaka aondoke katika nyumba hiyo.”

Hii ndio badali sahihi ambapo mtu anatakiwa kuomba ulinzi kwa maneno ya Allaah kamilifu kuliko kuwaomba ulinzi majini. Amesema (Ta´ala):

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ

”Sema: “Najikinga na Mola wa mapambazuko.”

Mapambazuko ni asubuhi. Mola wa mapambazuko ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Amesema (Ta´ala):

فَالِقُ الْإِصْبَاحِ

“Mpasuaji wa mapambazuko ya asubuhi.”[4]

Bi maana Mwenye kudhihirisha nuru ya asubuhi katika giza la usiku. Ni nani mwengine anayeyaweza haya kama si Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ

 “Najikinga na Mola wa mapambazuko.”

Mola wa mapambazuko kunapoingia asubuhi, mfalme na Mwenye kuuendesha na muweza wake.

أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ

“Najikinga na Mola wa mapambazuko.”

Hapa kumekusanywa shari za viumbe wote. Kwa hiyo mtu anaomba ulinzi kwa Allaah kutokamana na shari ya viumbe wote. Haya yanakutosha kutokamana na ulinzi aina zote au unajilinda kutokamana na yale yanayofanywa na watu.

مِن شَرِّ مَا خَلَقَ وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ

“Kutokamana na shari ya alivyoviumba na kutokamana na shari ya giza linapoingia.”

Ghaasik ni giza la usiku. Kwa sababu katika giza la usiku ndio mashaytwaan na wanyama wakali hutoka nje ambapo wewe unakuwa khatarini. Kwa hiyo unamwomba Allaah ulinzi kutokamana na giza hili na kutokamana na yaliyo ndani yake katika vitu hivi vyenye madhara.

وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَد

“Kutokamana na shari ya wapulizao mafundoni.”

Nao ni wale wachawi. Kwa hiyo unaomba ulinzi kwa Allaah kutokamana na uchawi na watu wake. Kwa sababu uchawi ni shari kubwa mno. Maneno Yake:

وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ

“Kutokamana na shari ya hasidi anapohusudu.”

Hasidi ni yule anayetamani neema iwaondokee wengine. Anapomuona mtu na neema basi anatamani imwondokee kwa sababu ya hasadi na uadui. Ni moja katika sifa mbaya kabisa. Kwa sababu ndani yake kuna kupingana na Allaah na vilevile ndani yake kuna kuwafanyia vibaya viumbe.

Kunaingia vilevile kijicho anayewasibu watu kwa kutazama kwake. Kwa sababu kuwasibu watu kwa kijicho ni aina fulani ya hasadi. Kwa hiyo wewe unamwomba Allaah kinga kutokamana na shari hizi. Kwa hiyo ikafahamisha kwamba kuomba ulinzi ni ´ibaadah ambayo haijuzu kumwelekezea mwengine asiyekuwa Allaah. Kwa msemo mwingine usiwatake ulinzi viumbe. Yule mwenye kuwataka ulinzi viumbe basi amemshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kumwambia ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Unapotaka ulinzi basi mtake ulinzi Allaah.”

[1] 113:01-02

[2] 72:06

[3] Muslim (2708).

[4] 06:96

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 147-149
  • Imechapishwa: 30/12/2020