69. Dalili kwamba kumtaka msaada Allaah ni ´ibaadah na aina mbili za kutaka msaada

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kutaka msaada ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.”[1]

Katika Hadiyth pia imekuja:

“Unapotaka msaada, basi mtake msaada Allaah.”[2]

MAELEZO

Kuna aina mbili za kutaka msaada:

Ya kwanza: Kutaka msaada kwa kitu ambacho hakiwezi yeyote isipokuwa Allaah. Kumfanyia aina hii asiyekuwa Allaah ni shirki. Mwenye kumtaka msaada mwengine asiyekuwa Allaah katika kitu ambacho hakiwezi yeyote isipokuwa Allaah amefanya shirki. Kwa sababu amefanya aina moja wapo ya ´ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall).

Ya pili: Kutaka msaada katika mambo ambayo kiumbe anayaweza. Unaweza kumtaka msaada mwenzako kujenga ukuta, kubeba mzigo au kukusaidia mahitajio ya halali. Amesema (Ta´ala):

وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖوَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ

“Saidiane katika wema na kumcha Allaah na wala msisaidiane katika dhambi na uadui.”[3]

Kutaka msaada katika mambo ya kawaida ambayo watu wanayaweza aina hii haina neno. Kwa sababu ni kusaidiana katika wema na kumcha Allaah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah yuko katika kumsaidia mja muda wa kuwa mja huyo yuko katika kumsaidia nduguye.”[4]

Ama kumtaka msaada kiumbe katika jambo ambalo haliwezi yeyote isipokuwa Allaah, kwa mfano kuleta riziki au kuzuia madhara, mambo haya hayawi isipokuwa kwa Allaah. Mifano mingine ni kuwataka msaada wafu, kuwataka msaada majini na mashaytwaan, kuwataka msaada viumbe wasioonekana ilihali hawakusikii ambapo unaita majina yao ni shirki kubwa. Kwa sababu unawataka msaada viumbe wasioweza kukusaidia. Amesema (Ta´ala):

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe pekee tunakuabudu na Wewe pekee tunakuomba msaada.”

Wewe pekee… – Hapa kumetangulizwa kitendo mbele ya mtendaji, jambo ambalo linafidisha ufupikaji.

Maana ya:

إِيَّاكَ نَعْبُدُ

”Wewe pekee tunakuabudu… “

Bi maana hatumwabudu mwengine asiyekuwa Wewe. Kwa hiyo ´ibaadah imefupika kwa Allaah (´Azza wa Jall).

وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“… na Wewe pekee tunakuomba msaada.”

Kutakwa msaada kumefupika kwa Allaah (´Azza wa Jall) katika mambo ambayo hayawezi yeyote isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Maneno Yake:

إِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“… Wewe pekee tunakuomba msaada.”

hapa mtu anajitakasa kutokamana na uwezo na uwezo na kwamba mtu hana nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah na wala hawezi isipokuwa kwa msaada wa Allaah (´Azza wa Jall). Hili ndio kusudio kubwa la kumwabudu Allaah pindi ambapo mja anajiweka mbali na shirki na anajiweka mbali na namna na nguvu. Hili ndio lengo kubwa la kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall).

[1] 01:05

[2] at-Tirmidhiy (2516).

[3] 05:02

[4] Muslim (2699).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 144-147
  • Imechapishwa: 30/12/2020