68. Dalili kwamba kurejea kwa Allaah ni ´ibaadah na muda ambao tawbah inakubaliwa kutoka kwa mja

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya kurejea ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ

“Rejeeni kwa Mola wenu na jisalimisheni Kwake kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa.”[1]

MAELEZO

Kurejea kuna maana ya kutubia. Kurejea na kutubia maana zake ni moja. Hata hivyo baadhi ya wanachuoni wamesema kuwa kurejea ni kitu maalum zaidi kuliko kutubia. Kwa msemo mwingine kurejea kuna msisitizo zaidi kwa sababu kumeambatana vilevile na kumwelekea Allaah (´Azza wa Jall). Bi maana ni tawbah maalum. Mtu anaweza kutubia, akaiacha dhambi, asiirudilie na akaijutia. Lakini anaweza kuwa na udhaifu inapokuja katika kumwelekea Allaah. Kurejea ni kule kumwelekea Allaah (´Azza wa Jall). Kwa ajili hii amesema:

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ

“Rejeeni kwa Mola wenu na jisalimisheni Kwake… “

Bi manaa rejeeni Kwake na mumwelekee Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala):

مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ

“… kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa.”

Itapokuja adhabu yenye kuangamiza basi haitokubali tawbah ya mwenye kutubia wakati huo:

إِلَّا قَوْمَ يُونُسَ لَمَّا آمَنُوا كَشَفْنَا عَنْهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ

“… isipokuwa watu wa Yuunus; walipoamini, basi tuliwaondoshea adhabu ya kutweza duniani.”[2]

Hawa wamevumiliwa. Vinginevyo kunapoteremka adhabu yenye kuangamiza haikubali tawbah. Kwa ajili hii akasema:

مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ

“… kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa.”

Tawbah na kurejea ni kitu kina muda uliowekewa mpaka. Tawbah ya anayezama au ya ambaye amefikiwa na kifo haikubaliwi. Wala haikubaliwi tawbah ya aliyeteremkiwa na adhabu yenye kuangamiza. Wala haikubaliwi tawbah pindi jua litapochomoza kutoka upande wa magharibi kabla ya kusimama kwa Qiyaamah. Kipindi hicho tawbah haikubaliwi. Allaah anawahimiza waja kufanya tawbah na kurejea Kwake kabla ya kumalizika muda wake:

مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ

“… kabla haijakufikieni adhabu kisha hamtonusuriwa.”

Kinacholengwa ni maneno Yake:

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ

“Rejeeni kwa Mola wenu… “

Ni dalili inayofahamisha kwamba kurejea ni aina fulani ya ´ibaadah. Kwa sababu amesema:

إِلَىٰ رَبِّكُمْ

“… kwa Mola wenu… “

Hii inafahamisha kuwa ni aina moja wapo ya ´ibaadah.

[1] 39:54

[2] 10:98

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 143-144
  • Imechapishwa: 29/12/2020