Imaam Yahyaa bin Sa´iyd al-Qattwaan

Yahyaa bin Sa´iyd bin Farruukh, imamu mkubwa, kiongozi wa waumini katika Hadiyth, Abu Sa´iyd at-Tamiymiy al-Baswriy al-Ahwal al-Qattwaan – hafidhi.

Alizaliwa mwaka 121.

Baadhi ya aliowasikia ni Sulaymaan at-Taymiy, Hishaam bin ´Urwah, Sulaymaan al-A´mash, Yahyaa bin Sa´iyd al-Answaariy, Ibn ´Awn, Shu´bah, ath-Thawriy, Muhammad bin ´ Ajlaan na wengine wengi.

Alitilia umuhimu jambo hili la elimu na akasafiri kwa ajili yake. Hifdhi iliishilia kwake. Amezungumza kuhusu kasoro [za Hadiyth] na wanamme. Watu wenye kuhifadhi wametokea katika chuo chake. Baadhi yao ni Musaddad, ´Aliy, al-Fallaas na wengineo. Katika mambo ya mataga alikuwa ni mwenye kufuata maoni ya Abu Haniyfah asipopata andiko.

Baadhi ya waliopokea kutoka kwake ni pamoja na Sufyaan, Shu´bah, ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy, Musaddad, Abu Bakr bin Abiy Shaybah, Ahmad, Ishaaq na wengineo.

Alikuwa akisema:

”Alilazimiana na Shu´bah kwa miaka 20.”

Imethibiti kwamba Ahmad bin Hanbal amesema:

“Sijawahi kumuona mtu kama Yahyaa bin al-Qattwaan.”

Yahyaa bin Ma´iyn amesema:

”´Abdur-Rahmaan alinambia: ”Hutoona kwa macho yako kama Yahyaa al-Qattwaan.”

´Aliy al-Madiyniy amesema:

”Sijaona mtu ambaye ni bingwa juu ya wanamme kama Yahyaa bin Sa´iyd.”

Bundaar amesema:

”Yahyaa bin Sa´iyd, imamu wa zama zake, ametuhadithia… ”

Abul-Waliyd at-Twayaalisiy amesema:

“Wamedai kuwa Yahyaa bin Sa´iyd ni mtumwa aliyeachwa huru na Banuu Tamiym. Alikuwa akiadhimishwa tangu akingali kijana.”

Ibn Ma´iyn amesema:

“Yahyaa bin Sa´iyd amenambia: “Mimi sio mtumwa wa yeyote.”

Ahmad bin Sa´iyd ad-Daarimiy ameeleza kuwa amemsikia Ahmad bin Hanbal akisema:

“Sijawahi kuandika Hadiyth kwa mtu mfano wa Yahyaa bin Sa´iyd.”

Abu Qudaamah as-Sarkhasiy amesimulia kuwa amemsikia Yahyaa bin al-Qattwaan akisema:

“Maimamu wote niliokutana nao walikuwa wakisema: “Imani ni maneno na vitendo, inazidi na inapungua.” Kadhalika walikuwa wanaonelea kuwa Jahmiyyah ni makafiri na pia wakimtanguliza Abu Bakr na ´Umar katika ubora na  ukhaliyfah.”

Haafidhw Ibn ´Ammaar amesema:

“Nilikuwa ninapomtazama Yahyaa al-Qattwaan, basi nafikiri kuwa hajui chochote kuhusu biashara za nguo. Lakini anapoanza kuzungumza, Fuqahaa´ wanamsikiza.”

Ahmad bin Muhammad bin Yahyaa al-Qattwaan amesema:

”Babu yangu kamwe hakuwa akifanya utani wala kucheka, isipokuwa tu kutabasamu. Kamwe hakuingia vyoo vya nje.”

´Aliy al-Madiyniy amesema:

”Tulikuwa nyumbani kwa Yahyaa bin Sa´iyd wakati bwana mmoja aliposoma Suurah ”ad-Dukhaan”. Ndipo Yahyaa akazimia na akaamshwa.”

Muhammad bin Sa´d amesema:

”Yahyaa alikuwa mwaminifu, mwenye kuaminiwa, yujuu na hoja.”

an-Nasaa´iy amesema:

”Chombo cha Allaah juu ya Hadiyth ni Shu´bah, Maalik na Yahyaa al-Qattwaan.”

Yahyaa bin Ma´iyn amesema:

”Yahyaa bin Sa´iyd hakuwahi kupitwa na swalah msikitini kwa miaka 40.”

 Shaadhdh bin Yahyaa ameeleza kuwa Yahyaa al-Qattwaan amesema:

”Yule mwenye kusema kuwa Suurah ”al-Ikhlaasw” imeumbwa ni zandiki.”

Muhammad bin Yahyaa bin Sa´iyd amesema:

”Baba yangu alinambia: ”Nilikuwa nikitoka nyumbani kwenda kutafuta Hadiyth na sirejei isipokuwa usiku.”

´Aliy al-Madiyniy amesema:

”Tulikuwa kwa Yahyaa bin Sa´iyd na wakati alipotoka nje ya msikiti, tukatoka pamoja naye. Alipofika kwenye mlango wa nyumba yake, akasimama na sisi tukasimama pamoja naye. Ndipo akamuona ar-Ruubiy akasema: ”Ingieni”, tukaingi. Halafu akamwambia ar-Ruubiy: ”Soma.”Alipoanza kusoma, nikamuona namna Yahyaa anavyobadilika mpaka alipofikia:

إِنَّ يَوْمَ الْفَصْلِ مِيقَاتُهُمْ أَجْمَعِينَ

”Hakika Siku ya hukumu ni wakati wao uliopangwa kwa wote.”[1]

Ndipo Yahyaa akazimia na sauti yake ikanyanyuliwa. Mlango ulikuwa karibu naye akajigonga kwenye mlango na ukakatika mgongo wake na hivyo damu ikaruka ambapo wanawake wakapiga makelele. Tukatoka nje ya mlango na tukasimama hapo mpaka wakati alipopata fahamu baada ya kitambo kidogo. Kisha tukaingia chumbani mwake na tukamkuta amelala juu ya godoro lake huku akisema:

إِنَّ يَوْمَ الْفَصْلِ مِيقَاتُهُمْ أَجْمَعِينَ

”Hakika Siku ya hukumu ni wakati wao uliopangwa kwa wote.”

Hakuacha kuendelea kuwa na sifa hiyo mpaka alipofariki – Allaah amrehemu.”

Wamesema kuwa Yahyaa bin Sa´iyd alikufa katika Safar mwaka 198, miezi minne kabla ya Ibn Mahdiy na Ibn ´Uyaynah – Allaah awarehemu.

Yahyaa bin Sa´iyd amesema:

”Usitazame Hadiyth, bali tazama cheni ya wapokezi. Ima cheni ya wapokezi iwe Swahiyh vinginevyo msije kudanganyika na Hadiyth ikiwa cheni ya wapokezi wake si Swahiyh.”

[1] 44:40

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (9/175-188)
  • Imechapishwa: 29/12/2020