Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya tisho ni Kauli Yake (Ta´ala):

فَلَا تَخْشَوْهُمْ

”Hivyo basi msiwaogope.”[1]

MAELEZO

Tisho ni aina fulani ya khofu. Ni kitu maalum zaidi kuliko khofu. Imesemwa pia kwamba tisho ni khofu inayotokana na utukuzaji. Amesema (Ta´ala):

فَلَا تَخْشَوْهُمْ وَاخْشَوْنِي

“Hivyo basi msiwaogope bali niogopeni.”[2]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameamrisha kumwogopa Yeye pekee. Amesema (Ta´ala) katika Aayah hiyo:

فَلَا تَخْشَوْهُمْ وَاخْشَوْنِي وَلِأُتِمَّ نِعْمَتِي عَلَيْكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ

“Basi msiwaogope bali niogopeni na ili Nitimize neema Yangu juu yenu na ili mpate kuongoka.”[3]

Kwa hiyo ameamrisha kumwogopa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Vilevile amesema kuhusu sifa za waswaliji:

وَالَّذِينَ هُم مِّنْ عَذَابِ رَبِّهِم مُّشْفِقُونَ

“Na wale wanaiogopa adhabu kutoka kwa Mola wao.”[4]

Bi maana wenye kukhofu. Hawa ni viumbe maalum wanaomwogopa Allaah (´Azza wa Jall). Amesema kuhusu Malaika:

يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ

“Wanamuogopa Mola wao Aliye juu yao na wanafanya yale wanayoamrishwa.”[5]

Viumbe maalum katika Malaika, Mitume, mawalii na waja wema wanakuwa na khofu ya hali ya juu kwa Allaah (´Azza wa Jall), kumwogopa Yeye na matumaini Kwake. Woga, khofu na tisho yote haya maana yake ni moja ingawa baadhi yazo ni maalum kuliko zengine. Walakini zinajumuishwa na kumwogopa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hizi ni miongoni mwa sifa za Mitume na waja wema wa Allaah. Ni aina kubwa miongoni mwa aina za ´ibaadah. Ni miongoni mwa matendo ya kimoyo ambayo hakuna anayeyajua isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

[1] 02:150

[2] 02:150

[3] 02:150

[4] 70:27

[5] 16:50

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 142-143
  • Imechapishwa: 29/12/2020