66. Dalili kwamba shauku, woga na unyenyekevu ni ´ibaadah na Radd kwa Suufiyyah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya shauku, woga na unyenyekeaji ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ

“Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri na wakituomba kwa matumaini na khofu na walikuwa Kwetu wenye kunyenyekea.”[1]

MAELEZO

Shauku – Ni kule kutafuta kitu chenye kusifiwa.

Woga – Ni kukhofu kitu kinachoogopwa. Amesema (Ta´ala):

وَإِيَّايَ فَارْهَبُونِ

“… na Mimi Pekee niogopeni.”[2]

Ni aina fulani ya khofu. Woga na khofu maana zake ni moja.

Unyenyekeaji – Ni aina fulani ya mtu kujidhalilisha na kunyenyekea mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni sehemu tukufu kabisa ya ´ibaadah. Maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّهُمْ

“Hakika wao… “

Dhamira inarudi kwa Mitume. Kwa sababu Allaah ametaja visa vya Mitume ndani ya Suurah “al-Anbiyaa´”:

إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ

“Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya kheri na wakituomba kwa matumaini na khofu na walikuwa Kwetu wenye kunyenyekea.”

Maneno Yake (Ta´ala):

يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ

“… wakikimbilia katika mambo ya kheri… “

Wanashindana kwayo na kuyakimbilia. Hizi ndio sifa za Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Hawahisi uvivu na wala kushindwa. Bali wanakimbilia katika kufanya mambo ya kheri na kushindana kwayo. Maneno Yake (Ta´ala):

وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا

“… na wakituomba kwa matumaini… “

hali ya kutamani yaliyoko kwa Allaah (´Azza wa Jall) na hali ya kutamani kufikia mahitajio. Maneno Yake (Ta´ala):

 وَرَهَبًا

“… na khofu.”

kwa kutuogopa sisi. Walikuwa wakimuomba Allaah awarehemu, wakimuomba asiwaadhibu, asiwachukulie na asiwaadhibu. Kwa hiyo walikuwa wakitumai huruma Yake na wakiogopa adhabu Yake. Amesema (Ta´ala):

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ

“Hao wanaowaomba [wao wenyewe] wanatafuta kwa Mola wao njia [na] kumkurubia kadri wanavyoweza na wanataraji rehema Zake na wanakhofu adhabu Yake.”[3]

Walikuwa wakimuomba Allaah hali ya kumwogopa na pia wakimuomba hali ya kutamani yale yaliyoko Kwake. Walikuwa wakimuomba Allaah awakadirie yaliyo na kheri na awaepushe na shari:

وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ

“… walikuwa Kwetu wenye kunyenyekea.”

Bi maana wakinyenyekea na wakijidhalilisha kwa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hiyo wakakusanya kati ya sifa tatu:

1- Matumaini.

2- Woga.

3- Unyenyekevu.

Hizi ndio sifa za Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Aina hizi tatu ni miongoni mwa aina za ´ibaadah kwa Allaah (´Azza wa Jall).

Ndani yake kuna Radd kwa Suufiyyah wanaosema kuwa hawamwabudu Allaah kwa sababu ya kutumai malipo Yake wala kuogopa adhabu Yake. Wanasema kuwa wanamwabudu kwa sababu ya kumpenda peke yake. Maneno haya ni batili. Kwa sababu Mitume wenyewe wanamuomba Allaah kwa kutumai na kwa kuogopa ilihali wao ndio viumbe wakamilifu zaidi.

[1] 21:90

[2] 02:40

[3] 17:57

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 140-142
  • Imechapishwa: 29/12/2020