Swali 66: Ni vipi ilikuwa hijjah ya kuaga?

Jibu: Imaam Muslim bin al-Hajjaaj amesema: Abu Bakr bin Abiy Shaybah na Ishaaq bin Ibraahiym wametuhadithia, kutoka kwa Haatim. Abu Bakr amesema: Haatim bin Ismaa’iyl al-Madaniy ametuhadithia, kutoka kwa Ja´far bin Muhammad, kutoka kwa baba yake ambaye amesema:

”Tuliingia kwa Jaabir bin ´Abdillaah ambapo akamuuliza mmoja baada ya mwingine mpaka alipofikia kwangu. Nikasema: ”Naitwa Muhammad bin ´Aliy al-Husayn.” Akaushusha mkono wake juu ya kichwa changu ambapo akafungua vifungo vyangu viwili vya juu kisha akaweka mkono wake katikati ya matiti yangu. Kipindi hicho nilikuwa mvulana mdogo. Akasema: ”Karibu, mpwa wangu! Uliza unachokitaka.” Nikamuuliza na alikuwa kipofu. Ulipofika wakati wa swalah akasimama, akiwa amejifunika blanketi yake. Kila alipoiweka mabegani mwake inapanda tena kutokana na udogo wake. Shuka yake ya juu ilikuwa pambizoni mwake kwenye kitu cha kuning´inizia nguo. Akatuswalisha. Nikasema: ”Tufahamishe juu ya hijjah yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).” Akaonyesha namba tisa kwa mkono wake na kusema: ”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ilimchukua miaka tisa kabla ya yeye kuhiji. Mwaka wa tisa watu wakatangaziwa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) atahiji. Watu wengi wakafika Madiynah. Kila mmoja anataka kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na wafanye kama alivofanya. Hivyo tukatoka naye mpaka tulipofika Dhul-Hulayfah ambapo akazaliwa Asmaa´ bint ´Umays Muhammad bin Abiy Bakr. Akamtumia ujumbe Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akimuuliza nini anachotakiwa kufanya. Akasema: ”Oga, zuia damu kisha uingie kwenye Ihraam.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaswali msikitini. Kisha akampanda Qaswaa´. Ngamia wake jike alipomchukua jangwani nilitazama na kuona wapanda farasi na watembea kwa miguu umbali ambao macho yangeweza kuona mbele yake, kulia kwake, kushoto kwake na nyuma yake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa kati yetu. Qur-aan ikiteremshwa kwake na yeye anajua tafsiri yake. Kile alichokifanyia kazi na sisi tulikifanyia kazi. Akaanza kwa Tawhiyd na kusema:

لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك، إن الحمد، والنعمة، لك والملك، لا شريك لك

”Nimekuitikia wito Wako, ee Allaah, nimekuitikia wito Wako. Nimekuitikia wito Wako, huna mshirika, nimekuitikia wito Wako. Hakika himdi, neema na ufalme ni Vyako. Huna mshirika.”

Watu wakafanya na kutangaza kama alivofanya. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakurudisha chochote katika yale waliyoyasema. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akalazimiana na tamko lake.”

Jaabir amesema:

”Hatunuii isipokuwa hajj tu, kwa sababu hatujui ´Umrah ni kitu gani. Wakati tulipofika katika Nyumba, akagusa pembe ambapo akachepua mizunguko mitatu na akatembea mizunguko mitatu. Halafu akaenda mahali aliposimama Ibraahiym (´alayhis-Salaam) na kusoma:

وَاتَّخِذُوا مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى

“Fanyeni mahali pa kusimama Ibraahiym kuwa ni sehemu ya kuswalia.”[1]

Alisimama kwa njia ya kwamba mahali pa kusimama na ile Nyumba vikawa mbele yake.”

Baba yangu akasema – na sijui kwamba amesimulia hilo kutoka kwa mwingine isipokuwa tu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Alisoma katika zile Rak´ah mbili Suurah ”al-Kaafiruun” na ”al-Ikhlaasw”.”

Kisha akatoka kupitia mlango kwenda Swafaa na kusoma:

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَآئِرِ اللّهِ

“Hakika vilima vya Swafaa na Marwah ni katika alama za Allaah.”[2]

na akasema:

”Naanza kwa kile alichoanza nacho Allaah.”

Akapanda Swafaa mpaka alipoiona Nyumba ambapo akakielekea Qiblah, akamuhimdi Allaah na kusema:

الله أكبر الله أكبر الله أكبر لا إله إلا الله وحده لا شريك له، له الملك وله الحمد ،يحيي و يميت وهو على كل شيء قدير، لا إله إلا الله وحده، أنجز وعده، ونصر عبده، وهزم الأحزاب وحده

”Allaah ni mkubwa. Allaah ni mkubwa. Allaah ni mkubwa. Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika. Ufalme na himdi zote njema ni Zake. Anahuisha na kufisha Naye juu ya kila jambo ni Muweza. Hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye. Ametimiza ahadi Yake, amemnusuru mja Wake na Yeye Mwenyewe amewashinda wale waliokula njama.”

Kisha akaomba baina ya hayo. Alikariri du´aa hiyo mara tatu. Kisha akashuka kwenda Marwah. Alipofika chini kwenye bonde akaanza kutembea kwa kasi hadi alipofika juu yake. Akaanza tena kutembea kawaida mpaka alipofika Marwah. Akafanya yaleyale aliyoyafanya Swafaa. Alipomaliza mzunguko wake Marwah akasema: “Lau ningefanya jambo ambalo hapo awali nililiacha, basi nisingechukua pamoja nami vichinjwa vya Hadiy. Badala yake ningezigeuza ´ibaadah hizo kuwa ´Umrah. Yeyote ambaye hajaleta vichinjwa vya Hadiy basi atoke katika Ihraam na kuigeuza ´ibaadah hiyo kuwa `Umrah.” Suraaqah bin Maalik bin Ja´sham akasimama na kusema: ”Ee Mtume wa Allaah! Linahusu mwaka huu peke yake au milele?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaingiza vidole vyake ndani ya vingine na kusema: ”´Umrah imeingia ndani ya hajj. ´ Umrah imeingia ndani ya hajj – bali milele.”

´Aliy akafika kutokea Yemen akiwa na vichinjwa vya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akamuona Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ametoka kwenye Ihraam, amevaa nguo za rangi na kutia wanja machoni. Akamkemea ambapo akasema: ”Baba yangu ameniamrisha hivo.” ´Aliy alikuwa akisema ´Iraaq: ”Nikaenda kwa Mtume wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumweleza yaliyofanywa na Faatwimah na kumuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu yale aliyomuhusisha nayo. Nikamweleza kuwa mimi nimemkemea kwa jambo hilo, ndipo akasema: “Amesema ukweli. Amesema ukweli. Nini ulichosema ulipomaliza hajj yako?” Nikasema: “Ee Allaah! Ninaingia kwenye hajj kwa yale aliyoingia kwayo Mtume Wako.” Akasema: “Nina pamoja nami wanyama wa Hadiy. Hivyo basi, usitoke kwenye Ihraam yako.” Kwa hivyo wanyama wa Hadiy ambao ‘Aliy alikuja nao kutoka Yemen na wanyama ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja nao wakawa mia moja. Watu wote wakatoka katika Ihraam na kukata nywele zao – wote isipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na wale waliokuwa wameleta vichinjwa vya Hadiy pamoja naye.

Siku ya Tarwiyah wakaenda Minaa. Wakaingia kwenye Ihraam kwa lengo la hajj. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akapanda farasi na akaswali Dhuhr na ‘Aswr, Maghrib na ´Ishaa, na Fajr hapo. Kisha akasubiri kidogo mpaka jua lilipochomoza. Alikuwa amejengewa kibanda kilichopambwa kwa manyoya huko Namirah.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaendelea safari yake. Quraysh hawakuamini jengine isipokuwa kwamba atasimama pale mahali Patakatifu, kama ambavo Quraysh walivyokuwa wakifanya katika zama za kabla ya Uislamu. Badala yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaendelea mpaka alipofika ´Arafah. Alipata kibanda chake huko Namirah na akapiga kambi hapo.

Baada ya jua kuzama, akaletewa Qaswaa’ na kuwekwa mbele yake. Akashuka bondeni, akawakhutubia watu na kusema: ”Hakika damu yenu na mali yenu ni haramu juu yenu kama utukufu wa siku yenu hii, katika mwezi wenu huu, katika mji wenu huu. Zindukeni! Hakika kila kitu katika yale mambo ya kipindi kabla ya kuja Uislamu yamefutwa chini ya miguu yangu. Damu ya kipindi kabla ya kuja Uislamu imefutwa. Damu ya kwanza ninayoifuta katika damu zetu ni damu ya Ibn Rabiy´ah bin al-Haarith. Alikuwa mwenye kunyonyeshwa kwa Banuu Sa´d ambapo akauliwa na Hudhayl. Ribaa ya kipindi kabla ya kuja Uislamu ni yenye kufutwa. Ribaa ya kwanza ninayoifuta katika ribaa zetu ni ribaa ya ´Abbaas bin ´Abdil-Muttwalib. Yote hayo yamefutwa. Mcheni Allaah juu ya wanawake. Kwani hakika mmewachukua kwa amana ya Allaah na mmehalalishiwa tupu zao kwa neno la Allaah. Hakika haki yenu juu yao ni kwamba wasimruhusu yeyote mnayemchukia kulala katika vitanda vyenu. Wakifanya hivo basi wapigeni kipigo kisichoumiza. Na haki yao juu yenu ni kuwahudumia na kuwavisha kwa wema. Nimekuacheni kile hamtopotea muda wa kuwa mtashikamana nacho barabara; Kitabu cha Allaah. Mtaulizwa juu yangu. Nini mtachosema?” Wakasema: ”Tunashuhudia ya kwamba umefikisha, umetekeleza na kunasihi.” Ndipo akaashiria kwa kidole chake cha shahaadah akikielekeza juu mbinguni: ”Ee Allaah! Shuhudia! Ee Allaah! Shuhudia! Ee Allaah! Shuhudia!”

Kisha kukaadhiniwa na kukimiwa ambapo akaswali Dhuhr. Kisha kukakimiwa akaswali `Aswr. Hakuna chochote alichoswali baina yake. Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akapanda kuelekea juu mpaka alipofika Mahali pa kusimama. Akafanya tumbo la ngamia wake Qaswaa´ kuielekea miamba, akasimama kwa njia kwamba awe na njia ya watembea kwa miguu mbele yake na akakielekea Qiblah. Aliendelea kusimama mpaka lilipozama jua, yakaondoka yale manjano na ikapotea ile diski yake. Usaamah akampanda farasi huyohuyo nyuma yake na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaondoka zake. Alivuta hatamu ya Qaswaa´ ili kichwa chake kiguse pedi ya sogi lake. Akaonyesha ishara kwa mkono wake wa kulia: “Enyi watu, tulieni, tulieni!” Kila alipofika kwenye milima ya mchanga, aliachia hatamu kidogo ili iweze kupanda juu.

Alipofika Muzdalifah akaswali Maghrib na ́Ishaa kwa adhaana moja na Iqaamah mbili. Hakuna chochote baina yake.

Halafu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akalala mpaka ilipopambazuka alfajiri. Akaswali Fajr wakati ilipombainikia kupambazuka kwa adhaana na Iqaamah moja. Kisha akampanda Qaswaa’. Alipofika mahali Patakatifu, akakielekea Qiblah na akaomba du´aa na kumkabiri. Alibaki katika hali hiyo mpaka kukawa na mwanga sana. Akaondoka kabla ya jua kuchomoza. al-Fadhwl bin ´Abbaas alimpanda farasi huyohuyo nyuma yake. Alikuwa ni mwanamme mwenye nywele nzuri, mweupe na mzuri. Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipoanza kumpanda farasi, waliwapitia wanawake wa Bahrain. al-Fadhwl akawatazama ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaweka mkono wake juu ya uso wa al-Fadhwl. Ndipo al-Fadhwl akageuza uso wake upande mwingine na kuendelea kuwatazama. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mara nyingine tena akageuza uso wa al-Fadhwl upande mwingine. Kisha al-Fadhwl akageuza uso wake tena upande mwingine na kuendelea kuwatazama.

Alipofika kwenye bonde la Muhassir, aliongeza kasi mwendo wake kidogo, kisha akashika njia ya katikati inayoelekea kwenye nguzo kubwa. Alipofika kwenye nguzo iliyosimama karibu na mti, akatupa kokoto saba. Kwa kila kokoto analotupa husema:

الله أكبر

”Allaah ni mkubwa.”

Baada ya hapo akatoka mpaka mahali pa machinjio. Yeye mwenyewe akachinja wanyama sitini na watatu kwa mkono wake. Kisha akamwacha ´Aliy achinje wanyama waliosalia na akamshirikisha katika uchinjaji wake. Kisha akaamrisha kipande cha nyama kichukuliwe kutoka kwa kila mnyama na kikapikwa ndani ya sufuria. Wote wawili wakala nyama yake na wakanywa mchuzi wake.

Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaendelea na safari yake kuelekea katika Nyumba. Akaswali Dhuhr huko Makkah. Alikuja kwa Banuu ´Abdil-Muttwalib wakimimina maji kutoka Zamzam akasema: “Mwagilia maji, ee Banuu ´Abdil-Muttwalib! Ingelikuwa sio kwa sababu ya watu kusongamana nanyi, basi mimi pia ningelimwagilia maji pamoja nanyi.” Wakampa ndoo ya maji ambapo akanywa humo.”[3]

Hadiyth hii ni kubwa na tukufu kuhusu taratibu za hajj. Isitoshe inayo misingi mingi ya dini na mambo ya kiimani. Kila mwanafunzi anatakiwa kuihifadhi, kuikariri, kuelewa maana yake na kuitendea kazi.

[1] 2:125

[2] 2:158

[3] Muslim (1218).

  • Mhusika: ´Allaamah Haafidhw bin Ahmad al-Hakamiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Amaaliy fiys-Siyrah an-Nabawiyyah, uk. 132-140
  • Imechapishwa: 01/11/2023