62. Dalili kwamba khofu ni ´ibaadah na mfano wa khofu ya shirki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya khofu ni Kauli Yake (Ta´ala):

فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi, mkiwa ni waumini.”[1]

MAELEZO

Khofu ni aina moja wapo ya ´ibaadah. Nayo ni ´ibaadah ya kimoyo. Vivyo hivyo khofu, woga, shauku, tisho, matarajio na utegemezi. Zote hizi ni ´ibaadah za kimoyo. Khofu ni kule mtu kujilinda na yenye kuchukiza. Khofu imegawanyika aina mbili:

1- Khofu ambayo ni ´ibaadah.

2- Khofu ambayo ni ya kimaumbile.

Aina ya kwanza ambayo ni khofu ya ´ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah ni shirki. Hayo yanakuwa kwa njia ya yeye kumwogopa mwengine asiyekuwa Allaah katika mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah. Kama mfano akamwogopa mwengine asimgonjweshe, akaipokonya roho yake au akamfisha mtoto wake, haya yanafanywa na wajinga wengi ambapo wanaogopa juu ya mimba za wake zao na watoto wao kutokamana na majini. Wanaowaogopa wachawi au wafu ambapo wakafanya matendo ya kishirikina ili waweze kusalimishwa kutokamana na khofu hii. Mambo haya hakuna ayawezaye isipokuwa Allaah pekee. Maradhi, kifo, riziki na kukata muda wa kuishi wa mtu ni mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall). Kadhalika kuteremsha mvua na mengineyo mfano wake ni mambo yasiyokuwa isipokuwa kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hiyo pindi mtu atapoogopa katika kitu kisichoweza yeyote isipokuwa Allaah ni shirki kubwa. Kwa sababu ni kufanya aina moja wapo ya ´ibaadah kwa asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall). Kama wale wenye kuyaogopa makaburi, majini na mashaytwaan wasije kuwagusisha baya au kuwateremshia madhara na matokeo yake wakaenda kujikurubisha katika vitu hivi kwa ajili ya kujilinda kutokamana na madhara yao au kwa ajili ya kuviogopa. Hii ni shirki kubwa. Wanasema kuwa wanaogopa wasipowachinjia basi watawasibu wao wenyewe, watoto wao, mali zao na mfano wa hayo. Hivo ndivo walivosema watu wa Huud:

إِن نَّقُولُ إِلَّا اعْتَرَاكَ بَعْضُ آلِهَتِنَا بِسُوءٍ

“Hakuna jengine tunachosema isipokuwa baadhi ya waabudiwa wetu wamekusibu kwa uovu.”

Wanamtisha na waungu wao na wanamtia khofu kwa waungu wao:

إِن نَّقُولُ إِلَّا اعْتَرَاكَ بَعْضُ آلِهَتِنَا بِسُوءٍ ۗ قَالَ إِنِّي أُشْهِدُ اللَّـهَ وَاشْهَدُوا أَنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ مِن دُونِهِ ۖ فَكِيدُونِي جَمِيعًا ثُمَّ لَا تُنظِرُونِ إِنِّي تَوَكَّلْتُ عَلَى اللَّـهِ رَبِّي وَرَبِّكُم

“Hakuna jengine tunachosema isipokuwa baadhi ya waabudiwa wetu wamekusibu kwa uovu. [Huud] akasema: “Hakika mimi namshuhudisha Allaah na shuhudieni kwamba mimi niko mbali kabisa na ambavyo mnashirikisha. Pasi Naye [Allaah] nifanyieni vitimbi nyote kisha msinipe muhula. Hakika mimi nimetegemea kwa Allaah, Mola wangu na Mola wenu.”[2]

Hii ndio Tawhiyd ambayo aliwapa kwayo changamoto wote na waungu wao.

فَكِيدُونِي جَمِيعًا ثُمَّ لَا تُنظِرُونِ

“… nifanyieni vitimbi nyote kisha msinipe muhula.”

Msiniache. Bali kuanzia sasa hivi. Hawakumuweza kwa chochote. Bali Allaah alimnusuru dhidi yao.

Kwa hiyo yule anayemwogopa asiyekuwa Allaah katika mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah ameshirikisha shirki kubwa. Hii inaitwa “shirki ya ´ibaadah”. Khofu ya shirki ni nyingi kwa watu ambapo wanayaogopa makaburi, mawalii, mashaytwaan na majini. Kwa ajili hiyo ndio maana wanawatangulizia vichinjwa, nadhiri, vyakula na pesa wanazorusha kwenye makaburi yao ili wasalimike kutokamana na shari yao au waweze kufikia kheri zao. Hii ndio khofu ya ´ibaadah.

[1] 03:175

[2] 11:54-56

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 132-135
  • Imechapishwa: 24/12/2020