Ni wajibu kutahadharisha wale watu wenye kujilipua

Swali: Tunatatizika juu ya suala la wale watakaowekwa Motoni kwa muda mrefu. Yule ambaye anajiua nafsi yake katika Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atadumishwa Motoni? 

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kwamba yule ambaye anaiua nafsi yake kwa chuma au sumu, basi ataadhibiwa kwacho ndani ya Moto kwa muda mrefu. Haya ameyasema kwa ajili ya kushtua. Kwa sababu mauaji mabaya ni yale ya mtu kujiua mwenyewe. Kwani mtu anatakiwa kuitetea nafsi yake zaidi ya ambavo anamtetea mwingine. Vipi basi mtu aiue nafsi yake mwenyewe? Kwa ajili hiyo ndio maana ni dhambi kubwa. Hivyo basi makusudio ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”kwa muda mrefu” ni kwa kutaka kushtua. Inafanana na maneno ya Allaah (Ta´aa): 

وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا

“Na yeyote atakayemuua muumini makusudi, basi malipo yake ni Moto hali ya kuwa ni mwenye kuwekwa humo kwa muda mrefu na Allaah atamghadhibikia na atamlaani na atamuandalia adhabu kuu.”[1]

Hapa inapata kubainika kwamba yale yanayofanywa na wale wenye kujilipua ambapo wanavaa vilipuzi, kama mabomu au vyenginevyo, na inakuwa wa mwanzo kufa ni wao wenyewe, wanaingia ndani ya matishio haya. Ni wenye kupata dhambi na ni wenye kutenda kosa kubwa. Lakini kwa kuzingatia kwamba ni watu wajinga na wenye ufahamu wa kimakosa, tunataraji kwamba hawaingii ndani ya matishio haya.

Lililo la wajibu kwetu ni kuwabainishia watu kwamba kitendo hicho si cha salama na kwamba ni haramu. 

Jambo la kushangaza ni kwamba baadhi ya watu wanajengea hoja kitendo hichi cha haramu, ambacho pia ni dhambi kubwa, kwa kitendo cha al-Baraa´ bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipozingirwa na ngome ya Musaylamah mwongo ambaye mlango wake ulikuwa umefungwa. Akawaomba wenzake wamtupe kwa ndani ili awafungulie wao mlango. Wakafanya hivo. Akaingia kwa ndani na akawafungulia mlango. Baadhi wanajengea hoja kisa hichi kwamba kujilipua ni jambo linalofaa. Hivi ndani yake kweli kuna dalili yoyote? Hakuna dalili yoyote. al-Baraa´ bin Maalik alibaki akiwa hai na huyu anayejilipua anakufa asilimia kwa mia. Kuhusu al-Baraa´ bin Maalik hakuiua nafsi yake. Ni kweli kwamba aliiweka nafsi yake khatarini, lakini kulikuweko pia na uwezekano wa kutokufa, kama ilivyotokea. Hakufa. Kitu ambacho ni mfano wa kisa cha al-Baraa´ bin Maalik ni mtu aingie kwa ujasiri kwenye safu za makafiri na akapambana kuliani na kushotoni. Lakini kuko uwezekano wa yeye kubaki hai. Kuhusu mtu ambaye anajiua, hakuna uwezekano wa yeye  kubaki hai.

Kwa ajili hiyo ni lazima kwetu kutosapoti matendo haya. Bali tunatakiwa kutahadharisha nao. 

[1] 04:93

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Bâb al-Maftuuh (170 B) Tarehe: 1418-07-13/1997-11-13
  • Imechapishwa: 24/12/2020