61. Du´aa ndio aina kubwa ya ´ibaadah na aina tatu za watu katika suala la ´ibaadah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika Hadiyth imekuja:

“Du´aa ndio kiini cha ´ibaadah.”[1]

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ

“Mola wenu Amesema: “Niombeni, Nitakuitikieni. Hakika wale wanaotakabari na ‘Ibaadah Yangu, wataingia Motoni hali ya kudhalilika.”[2]

MAELEZO

وَقَالَ رَبُّكُمُ

“Mola wenu Amesema.”

Bi maana Mola wenu amekuamrisheni.

أَسْتَجِبْ لَكُمْ

“Nitakuitikieni.”

Ameamrisha kumwomba Yeye (Subhaanah) na akaahidi kuitikia. Haya ni kutokana na ukarimu Wake (Subhaanah). Kwa sababu Yeye ni mkwasi kutokamana na du´aa zetu. Lakini sisi ni wenye kuhitajia kumwomba Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Anatuamrisha yale tunayohitajia na yanayotutengeneza. Yeye (Subhaanah) hukasirika tunapoacha kumwomba ilihali viumbe wanakasirika pindi unapowaomba. Kwa ajili hiyo mshairi amesema:

Allaah hukasirika unapoacha kumwomba

Mwanaadamu unapomwomba hukasirika

Mshairi mwingine amesema:

Lau watu wataombwa udongo wangelalamika

Wakiambiwa “leta” huchoka na kukataa

Watu wamegawanyika sampuli tatu:

Ya kwanza: Wasiomuomba Allaah kamwe. Hawa ni wenye kufanya kiburi juu ya kumwabudu Allaah.

Ya pili: Wenye kumuomba Allaah lakini wanawaomba wengine pamoja Naye. Hawa wanakuwa washirikina.

Ya tatu: Wenye kumuomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye du´aa. Hawa ndio wapwekeshaji.

Imepokelewa katika Hadiyth kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Du´aa ndio kiini cha ´ibaadah.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Du´aa ndio ´ibaadah.”[3]

Haya yanafahamisha ukubwa wa du´aa na kwamba ndio aina kubwa kabisa ya ´ibaadah. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… kiini cha ´ibaadah.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Du´aa ndio ´ibaadah.”

Upokezi wa pili ndio sahihi zaidi kuliko upokezi unaosema:

“Du´aa ndio kiini cha ´ibaadah.”

Lakini maana zake ni moja.

Hadiyth kwa upokezi wake inabainisha utukufu wa du´aa na kwamba ndio aina kubwa miongoni mwa aina za ´ibaadah. Ni kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“´Arafah ndio hajj.”[4]

Hiyo ina maana kwamba kusimama ´Arafah ndio nguzo kubwa ya hajj. Haina maana kwamba hajj yote ni ´Arafah. Lakini kusimama ´Arafah ndio nguzo kubwa ya hajj. Vivyo hivyo ´ibaadah haikufupika katika du´aa. Lakini du´aa ndio aina yake kubwa kabisa. Kwa ajili hii ndio maana akasema:

“Du´aa ndio ´ibaadah.”

kwa minajili ya kuitukuza du´aa na kubainisha nafasi yake.

Kisha Shaykh (Rahimahu Allaah) akataja baadhi ya mifano ya ´ibaadah ambayo ni: khofu, matarajio, utegemeaji, shauku [raghbah] na woga [rahbah], unyenyekeaji, tisho, kurejea [inaabah], kutaka msaada, kutaka kinga, kutaka kuokolewa, kuchinja, kuweka nadhiri na aina nyinginezo zote miongoni mwa aina za ´ibaadah ambazo Allaah Ameamrisha. Zote ziwe kwa ajili ya Allaah pekee.” Akasema (Rahimahu Allaah):

[1] at-Tirmidhiy (3371).

[2] 40:60

[3] Abu Daawuud (1479), at-Tirmidhiy (2969) na Ibn Maajah (3828).

[4] Abu Daawuud (1949), at-Tirmidhiy (779), an-Nasaa´iy (3016) na Ibn Maajah (3015).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 129-132
  • Imechapishwa: 24/12/2020