60. Dalili juu ya kwamba Allaah ameamrisha aabudiwe Yeye pekee

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Sehemu zote za kuswalia ni kwa ajili ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[1]

Mwenye kumtekelezea chochote katika hayo mwengine asiyekuwa Allaah ni mshirikina kafiri. Dalili ya hilo ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚإِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wowote juu ya hilo, basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake, kwani hakika hawafaulu makafiri.”[2]

MAELEZO

Misikiti – Husemwa neno “misikiti” na kukakusudiwa sehemu na maeneo ya kusujudia ambazo mtu anaswali ndani yake. Ndio maeneo yanayopendwa zaidi na Allaah (´Azza wa Jall). Kumepokelewa mahimizo ya kuijengea na kuiandaa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ambaye atajenga msikiti kwa ajili ya Allaah kama kijishimo cha ndege au mdogo zaidi basi Allaah atamjengea nyumba Peponi.”[3]

Allaah amesema:

إِنَّمَا يَعْمُرُ مَسَاجِدَ اللَّـهِ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ

”Hakika si venginevyo wanaoamirisha misikiti ya Allaah ni wale wanaomwamini Allaah na siku ya Mwisho.”[4]

Makusudio ya kuimarisha ni uimarishaji wa kihisia na wa kimaana. Watu wanatakiwa kuiimarisha kwa matofali na yale yanayohitajika ili waswaliji wahifadhike na yawafunike kutokamana na joto na yawalinde kutokamana na baridi. Kuiimarisha misikiti kwa ´ibaadah kama mfano wa swalah, usomaji wa Qur-aan na kumtaja Allaah (´Azza wa Jall).

Kunasemwa neno “misikiti” na kukakusudiwa viungo saba vya kusujudia: paji la uso, pua, mikono miwili, magoti mawili, kichwa na vidole vya miguu miwili. Kwa sababu viungo hivi vinamsujudia Allaah. Maana zote mbili zinaingia katika Aayah hii:

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ

“Sehemu zote za kuswalia.. “

Bi maana mahali panaposwaliwa na viungo vya sujuud ni kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall):

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[5]

Msiifanye misikiti hii na sehemu hizi ni pahali pa shirki na kumuomba asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall).  Bali ni lazima kuitakasa misikiti kutokamana na shirki. Ndani yake kusiwe makaburi, kuombwa asiyekuwa Allaah, Bid´ah na mambo mepya, duara zilizozuliwa za Suufiyyah.

Ni lazima kuisafisha misikiti kutokamana na Bid´ah, shirki na maasi kwa sababu ni ya Allaah (´Azza wa Jall). Kusiwe ndani yake isipokuwa tu yale yanayomridhisha Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hiyo usimwombe yeyote pamoja na Allaah katika misikiti hii au mkavitumia viungo vyenu vya sujuud kwa asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa sababu hii ni shirki kubwa kama ambaye analisujudia sanamu, kaburi au analisujudia sanamu. Huyu anamsujudia asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall).  Kinacholengwa ni katika maneno Yake:

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[6]

Ameamrisha kumtakasia du´aa Yeye pekee.

Yeyote – Inakusanya kila mwenye kuombwa badala ya Allaah (´Azza wa Jall) yeyote awaye. Ni mamoja ni Mtume, walii, mti au jiwe. Inamkusanya kila mwenye kuombwa badala ya Allaah (´Azza wa Jall) na inakuwa ni shirki kubwa.

[1] 72:18

[2] 23:117

[3] Ahmad (04/54) (2157), Ibn Maajah (738) na Ibn Khuzaymah (1292).

[4] 09:18

[5] 72:18

[6] 72:18

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 129
  • Imechapishwa: 24/12/2020