Swali: Ni ipi hukumu ya kuhifadhi picha za kivuli pamoja na kuzingatia kwamba mtu hakuzitundika juu ya kuta na amezihifadhi tu ndani ya albamu? Jengine ni kwamba hakuzipiga kwa ajili ya maadhimisho, lakini ni kwa ajili ya kumbukumbu.

Jibu: Kuhifadhi picha hizi ni jambo halijuzu. Hilo ni kwa sababu kuhifadhi picha kunafaa ikiwa ni kwa njia ya kuitweza kama zile zinazokuwa chini kwenye mazulia, mito, mapazia na mfano wake miongoni mwa vitu vinavyotwezwa. Picha kwenye vitu hivi zinafaa kwa mujibu wa wanachuoni wengi, japokuwa kuna tofauti. Lakini wanachuoni wengi wanaona kuwa inafaa.

Kuhusu picha ambazo hazitwezwi – ni mamoja zimetangaa na kutundikwa au zimefichikwa kama kwenye albamu – hazijuzu na wala haifai kwa mtu kuzihifadhi. Picha kwa ajili ya kumbukumbu ambazo zinawekwa ndani ya albamu au kwenginepo hazijuzu. Jengine ni kwamba mtu hatakiwi kutundika picha za kumbukumbu. Ni za kumbukumbu gani? Mtu huyu ambaye siku moja alikuwa ni mpendwa au rafiki yako siku miongoni mwa siku anaweza kuwa mwenye kukuchukia. Kwa ajili hii mtu hatakiwi kupitiliza katika mapenzi wala katika kuchukia. Picha hizi za kumbukumbu hazitakiwi. Bali haijuzu kwa mtu akazihifadhi.

Kuhusu picha kuna aina mbili ya picha:

1- Kuchora kwa mkono kwa njia ya kwamba mtu akachora picha ya mwili ikiwa na uso, mikono miwili na viungo vyenginevyo. Jambo hili halifai nalo ndilo ambalo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani yule mwenye kulifanya na akaeleza kuwa mwenye kufanya hivo ni miongoni mwa watu wataokuwa na adhabu kali kabisa.

2- Kuchukua picha kwa vifaa vya kisasa. Hapa ndipo wanachuoni wametofautiana. Hilo ni kwa sababu picha kwa kunakili sio picha iliotengenezwa na mtengenezaji. Huo ndio uhakika wa mambo. Amenakili picha na sio mtengeneza picha. Kuna tofauti kati ya mtengeneza picha ambaye anataka kuvumbua na kufanya usanifu na matokeo yake ionekane natija ya kazi yake na mipango na uumbaji wake kama uumbaji wa Allaah (´Azza wa Jall) na kati ya mtu mwenye kunakili ambaye ananukuu yale aliyotengeneza Allaah kupitia kivuli. Kuna tofauti kati ya hayo mawili. Kwa ajili hii endapo utaniletea kijitabu na ukaniomba nikuhamishie maandishi kutoka humo kwenda sehemu nyingine na nikafanya hivo, katika hali hii yale maandishi yatakuwa ni yangu. Lakini iwapo utanambia nichukue kijitabu hicho na nikupigie nacho picha/kopi kwa kifaa cha kisasa ambapo nikafanya hivo, hapo nitakuwa mwenye kukopi na kijitabu hichi cha kopi kitakuwa vilevile kama kile kijitabu chako cha asili. Kitabu hichi cha pili hakitokuwa kama kile kilichoandikwa kwa hati ya mkono. Haya ndio ambayo tunayapa nguvu ya kwamba picha hizi za kisasa hazina neno. Lakini kunatakiwa kutazamwa ni yepi malengo yake? Ikiwa malengo ni kuhifadhi picha hizi kwa njia isiyoruhusiwa, basi itakuwa ni haramu kwa upande huo. Hapo itakuwa ni uharamu wa njia na si uharamu wa malengo. Ama ikiwa malengo ni kwa ajili ya maslahi fulani kama kuchunga amani katika wilaya na mfano wake hakuna neno. Pamoja na kwamba tumeyapa nguvu maoni yanayosema kuwa inafaa tunaona kuwa linalomstahikia muislamu ni yeye ajitenge na jambo hilo. Kufanya hivo ndio kumcha Allaah zaidi na kujichunga kutokana na ile shubuha inayopatikana ndani yake. Kwani wanachuoni wengine wanaona kuwa picha, kukiwemo zile za kivuli au za vifaa vya kisasa, ni haramu. Mtu anapaswa kuacha kile ambacho ni haramu. Isipokuwa haja ikipelekea kufanya hivo. Chenye kutatiza kinaondoka kwa sababu ya haja.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (12) http://binothaimeen.net/content/6763
  • Imechapishwa: 23/12/2020