1- Baqiyyah amepokea kutoka kwa Muhammad bin Ziyaad ambaye amesema:

“Mwanamke mmoja alimuharibia mke wa Abu Muslim ambapo akamuombea du´aa mbaya na hivyo akawa kipofu. Mwanamke yule akamjia, akakubali na kutubu. Akasema: “Ee Allaah! Kama ni mkweli basi nakuomba mrudishie macho yake.” Macho yake yakarudi.”[1]

2- Bilaal bin Sa´d amesema:

“Tetesi za ´Aamir bin ´Abdi Qays zilifika kwa Ziyaad. Watu wakasema: “Hapa tuko na mwanamme ambaye hunyamaza pindi anapoambiwa kuwa yeye ni bora kuliko Ibraahiym (´alayhis-Salaam) na anajiweka mbali na wanawake.” Ziyaad akatuma ujumbe kuhusu bwana huyo kwa ´Uthmaan na ´Uthmaan akamrudishia: “Mtume Shaam juu ya kibanda cha ngamia.” Wakati barua ilipofika ´Aamir akaletwa. Akasema: “Wewe ndiye mwenye kunyamaza pindi unapoambiwa kuwa ni mbora kuliko Ibraahiym (´alayhis-Salaam)?” ´Aamir akasema: “Naapa kwa Allaah kwamba haikuwa kunyamaza kwangu isipokuwa ni kwa sababu ya mshangao. Natamani lau ningekuwa vumbi ya miguu yake.” Akauliza: “Unajitenga mbali na wanawake?” ´Aamir akajibu: “Naapa kwa Allaah kwamba sikujiweka mbali nao isipokuwa ni kwa sababu jambo hilo linapelekea katika kupata mtoto na kutenganisha na ulimwengu. Ndio maana napenda kuwa peke yangu.”[2]

3- Qataadah amesema:

“´Aamir bin ´Abdi Qays alikuwa akimuomba Mola wake kumwondoshea ndani ya moyo wake matamanio ya wanawake. Alikuwa si mwenye kutikiswa ni mamoja amekutana na mwanamme au mwanamke. Alimwomba vilevile Mola wake kumzuilia moyo wake kutokamana na shaytwaan pindi amesimama na kuswali, lakini du´aa hiyo haikupokelewa.”[3]

Imesemekana vilevile kwamba tatizo hilo lilimwondoka pia.

4- ´Aliy bin Swaalih ameeleza:

“Suwayd bin Ghafalah alifikisha miaka 120 na kamwe hakuwahi kuonekana akiketi chini kwa kuisimamisha miguu yake dhidi ya kifua wala mwenye kuegemea kitu. Alimuoa bikira.”[4]

Bi maana katika mwaka huohuo aliokufa ndani yake.

5- ´Aaswim bin Kulayb amesema:

“Suwayd bin Ghafalah alimuoa bikira wakati alipokuwa na miaka 116.”[5]

6- al-Ahnaf amesema:

“Viepusheni vikao vyetu kuwataja wanawake na chakula. Mimi namchukia mwanamme anayeelezea tupu yake na tumbo lake.”[6]

7- al-Ahnaf amesema:

“Nimesikia Khutbah ya Abu Bakr, ´Umar na makhaliyfah wengine lakini sijawahi kusikia maneno ya kiumbe yaliyo makubwa na mazuri zaidi kama ya mama wa waumini ´Aaishah.”[7]

8- Zayd bin Aslam ameeleza kwamba baba yake Aslam amesema:

“Alikuwa ´Umar pindi anaponituma kwa mmoja katika watoto wake basi anasema: “Usimjuze ni kwa nini nimekutuma” kwa kuchelea Shaytwaan asije kumfanya akasema uongo. Siku moja akaja mke wa ´Ubaydullaah bin ´Umar na kusema: “Abu ´Iysaa hanihudumii si chakula wala mavazi.” ´Umar akasema: “Ni nani Abu ´Iysaa?” Mwanamke yule akasema: “Mwanao.” Akasema: “Kwani ´Iysaa anaye baba?” Hivyo akaniagiza kwake na akanambia: “Usimweleze kitu.” Nilipofika kwake nikamkuta ´Abdullaah yuko na jogoo na kuku. Nikasema: “Itikia wito wa baba yako.” Akasema: “Anataka nini?” Akasema: “Amenikataza nisikwambie.” Akasema: “Mimi nitakupa jogoo na kuku.” Nikamshurutishia asimwambie kitu ´Umar ambapo nikamweleza aliyosema. Amenipa jogoo na kuku. Nilipofika kwa ´Umar akaniuliza: “Umemwambia?” Naapa kwa Allaah sikuweza kumwambia ´hapana` ndipo nikasema: “Ndio.” Akaniuliza: “Amekupa hongo?” Nikasema: “Ndio.” Akanikamata kwa mkono wake wa kushoto na akaanza kunichapa bakora na nikawa naruka huku na kule. Akasema: “Unatakiwa kuchapwa bakora.” Kisha akasema: “Kun-ya yako ni Abu ´Iysaa? Je, ´Iysaa anaye baba?”[8][9]

9- Abu Qilaabah amesema:

“Bwana mmoja alikutana na ´Aamir bin ´Abdi Qays akasema: “Kitu gani hiki? Allaah si amesema:

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ وَجَعَلْنَا لَهُمْ أَزْوَاجًا وَذُرِّيَّةً ۚ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Kwa hakika tuliwatuma Mitume kabla yako na tukawafanya kuwa na wake na kizazi. Na haiwi kwa Mtume yeyote kuleta ishara yoyote isipokuwa kwa idhini ya Allaah.”[10]

´Aamir akajibu: “Allaah pia si amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu.”[11]

10- ash-Sha´biy amesema:

“Siku moja Masruuq alipoteza fahamu. Wakati alipokuwa mtoto ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alikuwa amemuasili na hivyo akamwita msichana wake ´Aaishah. Daima alikuwa anamtii msichana wake. Akashuka kwa ajili yake na kusema: “Ee baba yangu kipenzi! Kata swawm na unywe maji.” Akasema: “Kipi kilichokufanya unambie hivo?” Msichana yule akasema: “Kukujali.” Akasema: “Nafunga kwa sababu ya kuijali nafsi yangu juu ya Siku ambayo inalingana na miaka 50.000.”

[1] 4/11.

[2] 4/16.

[3] 4/17.

[4] 4/72.

[5] 4/72.

[6] 4/94.

[7] 4/95.

[8] 4/99-100.

[9] Ibn ´Asaakir amesema: ”Anayezungumzishwa hapa ni ´Ubayduullaah.” (Nihaayat-ul-Khabar (2/408))

[10] 13:38

[11] 51:56 4/17.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’
  • Imechapishwa: 23/12/2020