59. Mfano wa aina za ´ibaadah alizoamrisha Allaah II

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Miongoni mwa hizo ni du´aa pia, khofu, matarajio, utegemeaji, shauku [raghbah] na woga [rahbah], unyenyekeaji, tisho, kurejea [inaabah], kutaka msaada, kutaka kinga, kutaka kuokolewa, kuchinja, kuweka nadhiri na aina nyinginezo zote miongoni mwa aina za ´ibaadah ambazo Allaah ameamrisha. Zote ziwe kwa ajili ya Allaah pekee. 

MAELEZO

Miongoni mwa hizo ni du´aa – Bi maana miongoni mwa aina za ´ibaadah ni du´aa. Ameanza kwayo kwa sababu ndio aina kubwa ya ´ibaadah. Du´aa imegawanyika aina mbili:

1- Du´aa ya ´ibaadah.

2- Du´aa ya kuomba.

Du´aa ya ´ibaadah ni kule kumsifu Allaah kama ilivyo mwanzoni mwa al-Faatihah:

الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Mfalme wa siku ya malipo. Wewe pekee tunakuabudu na Wewe pekee tunakuomba msaada.”[1]

Hii yote ni du´aa ya ´ibaadah.

اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ

“Tuongoze njia iliyonyooka; njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea.”[2]

Hii ni du´aa ya kuomba.

Du´aa ya kuomba ni kule kuomba kitu kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa mfano mtu kuomba uongofu, riziki, kuomba elimu kutoka kwa Allaah na kuomba kuafikishwa.

[1] 01:01-05

[2] 01:06-07

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 127
  • Imechapishwa: 27/12/2020