58. Mfano wa aina za ´ibaadah alizoamrisha Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mfano wa aina za ´ibaadah ambazo Allaah ameamrisha ni Uislamu, Imani na Ihsaan.

MAELEZO

Shaykh (Rahimahu Allaah) ameleta mifano ya ´ibaadah kwa njia ya kupigia mfano na si kwa njia ya ufupikaji. Kwa sababu ni zaidi ya alizotaja. Haiwezekani kuziorodhesha katika kujitabu kidogo. Lakini ameleta mifano tu. Shaykh-ul-Islaam ana kitabu cha kujitegemea kwa jina “al-´Ubuudiyyah” kinachotafiti mambo ya ´ibaadah, aina zake na ubainifu wa upondokaji uliyofanywa na Suufiyyah na wengineo katika ´ibaadah. Ni kitabu muhimu ambacho mwanafunzi anahitajia kukisoma. Maneno yake (Rahimahu Allaah):

“Mfano wa Uislamu, imani na Ihsaan.”

Haya matatu ndio aina kubwa za ´ibaadah; Uislamu, imani na ihsaan. Maelezo yake yatakuja katika maneno ya Shaykh (Rahimahu Allaah) katika msingi wa pili. Ameyataja hapa kwa sababu ni miongoni mwa aina za ´ibaadah.

Uislamu kwa nguzo zake tano: shahaadah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji nyumba tukufu ya Allaah. Yote haya ni ´ibaadah za kimwili na za kimali.

Vivyo hivyo nguzo sita za imani: kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na kuamini Qadar kheri na shari yake. Hizi ni ´ibaadah za kimoyo.

Vivyo hivyo Ihsaan ambayo ina nguzo moja: Kumwabudu Allaah kama vile unamuona na ikiwa wewe humuoni basi tambua kuwa Yeye anakuona. Hii ndio ´ibaadah iliyo juu zaidi. Kwa sababu Ihsaan ndio aina ya juu kabisa ya ´ibaadah.

Mambo haya ndio huitwa ngazi za dini. Kwa sababu mkusanyiko wa yote hayo ndio dini. Kwa sababu Jibriyl alipomuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mbele ya Maswahabah zake baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumjibu juu ya Uislamu, imani na Ihsaan akasema:

“Huyu ni Jibriyl. Amekujieni kukufunzeni jambo la dini yenu.”[1]

Kwa hiyo mambo haya matatu yakaitwa ndio dini.

[1] al-Bukhaariy (4777) na Muslim (08, 09 na 10).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 124-127
  • Imechapishwa: 23/12/2020