4 – Miongoni mwa vitu vinavyoweza kutumiwa ni kanuni isemayo njia ina hukumu moja kama malengo. Miongoni mwa mambo yanayofungamana na hoja hiyo ni kwamba vile vinavyotumika wakati wa kulingania kwa Allaah (Ta´ala) vinafanya njia inayofikia katika lengo la ulinganizi, navyo ni kuwalingania na kuwarekebisha watu. Maadamu njia ni yenye kusifiwa kwa mtazamo wa Shari´ah, basi mfumo wake unachukua hukumu hiyohiyo. Kwa hivyo mfumo pia unakuwa wenye kusifiwa kwa mujibu wa Shari´ah.

Ndio, lakini haimaanishi kila njia na mfumo – ijapo utakuwa wa haramu –itakuwa nzuri kwa sababu tu unatumiwa kwa lengo zuri.Vinginevyo yafutwe yote yaliyomo ndani ya Qur-aan na Sunnah na matamanio ya mtu ndio yawe mwongozo wa matendo. Katika hali hiyo vichukuliwe vilivyo haramu katika kumtibu mgonjwa, kula ribaa na kuvaa nguo ilio chini ya kongo mbili za miguu kwa ajili ya kulingania na kadhalika. Maana sahihi ya kanuni hiyo, ni kwamba mfumo kwa nisba ya lengo zuri ni lazima uwe unakubalika katika Shari´ah – wa lazima, unaopendeza, unaoruhusiwa au pengine ukawa wenye kuchukiza, lakini usiwe wa haramu. Pili ni kwamba kanuni hii haichukuliwi moja kwa moja kama ilivyo. Mfumo unaweza kuwa wenye kuchukiza au wa haramu tofauti na inapokuja katika lengo lake. ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema wakati alipokuwa anathibitisha kuwa kutikisika kwa ulimi kwa maneno hakulingani, bali ima wenye kushinda nguvu au wenye kushindwa nguvu:

“Ikisemwa ikiwa kitendo – bi maana lengo – linalingana, basi kitendo cha ulimi, ambacho ndio mfumo, kitakuwa hivyo, kwa sababu mfumo una hukumu moja kama lengo, jibu ni kwamba hailazimu iwe hivyo. Kitu kinaweza kuwa chenye kuruhusiwa na pengine cha wajibu lakini njia yake ikawa inachukiza. Mfano wa hilo ni kutimiza nadhiri kwa lengo la kufanya ´ibaadah; ni lazima kuitimiza ijapo njia yake – nayo ni nadhiri – inachukiza na kukatazwa. Kadhalika kiapo kinachochukiza[1] ni chenye nguvu licha ya kwamba ni lazima ima kukitekeleza au kukitolea kafara. Vivyo hivyo kuwaomba watu wakati mtu anahitaji ni jambo linachukiza, lakini inafaa kunufaika na kile alichokipata. Kuna mifano mingi kama hiyo. Mfumo unaweza kuwa na uharibifu wenye kuchukiza au wenye kuharamishwa na lengo lake lisiwe la haramu wala la kuchukiza.”[2]

[1] Kama mwenye kuapa kufanya jambo linalochukiza au kuacha jambo linalopendeza.

[2] Madaaridj-us-Saalikiyn (1/116). Tazama ”al-Furuuq” (2/32-33) ya al-Qaraafiyna ”al-Qawaa´id” (2/394) ya al-Muqriy.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 89-90
  • Imechapishwa: 30/05/2023