Swalah inayopendeza nyuma ya anayeswali faradhi

Je, ni sahihi kuswali swalah ya faradhi nyuma ya anayeswali swalah inayopendeza au kinyume chake? Kuhusiana na mtu mwenye kuswali swalah inayopendeza nyuma ya anayeswali faradhi ni sawa. Sunnah imesapoti hilo. Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alienda katika msikiti wa al-Khayf Minaa katika swalah ya Fajr na akakutana na watu wawili wasioswali. Akawauliza: “Ni kipi kimechowafanya kutoswali na wenzenu?” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tumeswali majumbani mwetu.”

Inawezekana waliswali majumbani mwao kwa kufikiria kuwa hawatowahi swalah ya mkusanyiko au kuna uwezekano kukawa sababu nyingine. Akasema:

“Mnaposwali majumbani mwenu kisha mkaja katika mkusanyiko msikitini, basi pamoja na wenzenu. Hiyo itahesabika ni swalah ya sunnah kwenu.”[1]

Maneno yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)

“Hiyo itahesabika ni swalah ya sunnah kwenu.”

kunamaanishwa hiyo swalah ya pili kwa kuwa ile ya kwanza wameshatekeleza wajibu wao wa kuswali faradhi na imeshapita hiyo.Kwa hiyo, ikiwa maamuma ndiye mwenye kuswali swalah inayopendeza na imamu ndio anaswali faradhi, ni sawa. Hilo limefahamishwa na Hadiyth hii.

Vipi kinyume chake ikiwa imamu anaswali swalah inayopendeza na maamuma anaswali faradhi? Mfano wa karibu wa hilo katika siku za Ramadhaan. Mtu ameingia msikitini na ´Ishaa imeshampita akakuta watu wanaswali Tarawiyh. Je, aingie pamoja nao kwa nia ya ´Ishaa au aswali faradhi peke yake kisha ndio aingie pamoja nao kwa nia ya Tarawiyh? Hapa wanachuoni wamekinzana:

1 – Kuna waliosema kuwa si sahihi kuswali faradhi nyuma ya anayeswali swalahinayopendeza. Swalah ya faradhi ina hadhi zaidi. Haiwezekani swalah ya maamuma ikawa na hadhi zaidi kuliko swalah ya imamu.

2 – Wengine wakasema kuwa ni sahihi kuswali faradhi nyuma ya swalah inayopendeza. Kumethibiti hilo katika  Sunnah. Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa akiswali pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) swalah ya ´Ishaa kisha anaenda kwa watu wake na kuwaswalisha swalah hiyo. Kwake inahesabika kuwa ni swalah inayopendeza na kwao [anaowaswalisha] ni faradhi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumkataza kufanya hivo…

Kwa hivyo sahihi ni kwamba inajuzu kwa mtu kuswali faradhi nyuma ya anayeswali swalah ya inayopendeza.

[1] Abu Daawuud (575).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/383-385)
  • Imechapishwa: 29/05/2023