60. Mambo yaliyoibahishwa yanaweza kuwa ´ibaadah

Wanazuoni wengine wakaona kuwa nia njema inayageuza mambo yaliyoibahishwa kuwa ´ibaadah anayolipwa thawabu mwenye nayo. Ibn-ul-Haaj amesema:

“Mambo yaliyoibahishwa, kwa nia, yanakuwa yenye kupendeza.”[1]

Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema kuwa wafanya ´ibaadah bora ni wale ambao wameyageuza mambo yao yaliyoibahishwa kwenda katika utiifu na ´ibaadah kutokana na nia zao; kwao mambo yaliyoibahishwa hayalingani, bali daima yanakuwa na nguvu[2].

Shaykh ´Umar al-Ashqar amesema baada ya kutaja maoni yote mawili:

“Inaweza kuonekana kwamba kuna mgongano katika maoni haya mawili, lakini yule mwenye kufikiria kwa kina ataona kuwa kile kilichopingwa na maoni ya kwanza sio kilichothibitishwa na maoni ya pili. Maoni ya kwanza yanapinga mambo yaliyoibahishwa kugeuka kwenda katika ´ibaadah, jambo ambalo ni haki ambayo haijuzu kwa yeyote kuonelea kinyume chake. Yule anayedhani kuwa anamwabudu Allaah kwa kutembea, kusimama au kwa mavazi meusi au ya kijani amekosea kwa sababu mambo haya kwa dhati yake sio ´ibaadah. Kwa hiyo wanachotaka kusema watetezi wa maoni haya ni kwamba mambo yaliyoibahishwa yenyewe kama yenyewe sio ´ibaadah kama ilivyo swalah, kisomo cha Qur-aan na zakaah. Watetezi wa maoni ya pili wanaosema kuwa mambo yaliyoibahishwa yanaweza kuwa ´ibaadah makusudio yao sio makusudio ya wale watetezi wa maoni ya kwanza. Shaykh-ul-Islaam (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mtu hatakiwi kufanya mambo yaliyoibahishwa isipokuwa yale yanayomsaidia katika utiifu na akakusudia yamsaidie juu ya kumtii Allaah.”[3]

Ibn-ush-Shaat amesema:

“Mtu akikusudia kwa mambo yaliyoibahishwa kupata nguvu au kufikia utiifu, inakuwa ni ´ibaadah. Mfano wa mambo hayo ni kula, kulala na kuchuma mali.”[4]

Kwa hiyo muislamu akikusudia kwa kulala kwake, kula kwake na kunywa kwake kupata nguvu juu ya kumtii Allaah ili aweze kusimama usiku kuswali na kupambana katika njia ya Allaah, analipwa thawabu kwa matendo haya kutokana na nia hii. Muislamu akifanya kitu kilichoibahishwa huku akiona kuwa Allaah amemuhalalishia nayo, kama ambaye anamjamii mke wake kwa kukusudia kuyaepuka mambo ya haramu, basi analipwa thawabu, kama ilivyokuja katika Hadiyth ya Abu Dharr iliyotangulia ambayo imepokelewa na Muslim.

Kitu kinaweza kuwa kimeibahishwa kwa kiasi lakini kinahitajika kikamilifu. Inafaa kwa mtu kuacha kula, kunywa na kupambana na nafsi yake katika baadhi ya nyakati, hata hivyo haifai kufanya hivo kwa njia ya kudumu mpaka akaiangamiza nafsi yake. Kwa ajili hiyo kikosi kikubwa cha wanazuoni wamemuwajibishia mtu mwenye dharurah kula nyamafu na wakachelea kuadhibiwa ikiwa ataacha kula mpaka akaangamia.”[5]

Kwa haya imebainika kuwa ni kweli mambo yaliyoibahishwa yanaweza kuwa yenye kupendeza kutokana na nia njema, lakini kujengea hoja kitu hicho juu ya kusihi kuzua njia ya kulingania kwa njia ya ´ibaadah ni jambo la batili. Tumekwishatangulia kutaja kwamba Bid´ah inaweza kuingia katika mambo ya kiada kama inavyoweza kuingia katika mambo ya ki-´ibaadah.

[1] al-Madkhal (1/21-22).

[2] Tazama ”Madaarij-us-Saalikiyn” (1/107).

[3] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/460-461).

[4] Ghamz ´Uyuun-il-Baswaair (1/34).

[5] Maqaaswid-ul-Mukallafiyn, uk. 493-497, kwa baadhi ya mageuzi.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 88-89
  • Imechapishwa: 29/05/2023