59. Mambo yaliyoibahishwa hayawezi kuwa ´ibaadah

3 – Hoja tata nyingine inayoweza kutumiwa ni kwamba mambo yaliyoibahishwa yanaweza kubadilishwa, kutokana na nia, kwenda katika ´ibaadah ambayo mtu analipwa thawabu kwayo. Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika hutotoa matumizi yoyote ambayo kwayo unatafuta kuona uso wa Allaah isipokuwa utalipwa thawabu kwayo mpaka kile unachokiweka kwenye mdomo wa mwanamke wako.”[1]

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… mmoja wenu kufanya jimaa na mke wake ni swadaqah.” Wakasema: “Ee Mtume wa  Allaah! Mmoja wetu anayaendea matamanio yake kisha analipwa thawabu kwayo?” Akasema: “Mnaonaje endapo atayaweka matamanio yake kwenye [tupu ya] haramu si atapata dhambi? Basi vivyo hivyo akiyaweka kwenye [tupu ya] halali analipwa thawabu.”[2]

Kwa maana hiyo, wanasema watetezi kwamba mtu awe na nia njema kwa njia hizi zilizozuliwa na zilizoibahishwa ili mtu aweze kulipwa thawabu kwazo.

Mosi ni kwamba tunatakiwa kuweka wazi suala la mambo yaliyoibahishwa na nia. Baada ya hapo tutabainisha kuanguka na ubatili wa hoja hii.

Wanazuoni wametofautiana juu ya kubadilika vitu vilivyoibahiswa kwenda katika ´ibaadah kwa nia njema. Baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa vitu vilivyoibahishwa haviwezi kuwa ´ibaadah, hivyo kuweka nia hakuna maana yoyote[3]. al-Hattwaab amesema:

“Shari´ah yote ima iwe ni mambo yanayotakikana au mambo yaliyoibahishwa. Mambo yaliyoibahishwa hayawezi kuwa ´ibaadah, kwa hiyo nia haina nafasi mahali hapa.”[4]

Ili kupitisha maoni yake wanazuoni wa Maalikiyyah wamejengea hoja kwa Aayah ifuatayo:

وَلَيْسَ الْبِرُّ بِأَن تَأْتُوا الْبُيُوتَ مِن ظُهُورِهَا وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنِ اتَّقَىٰ

“Na si wema kuingia nyumba kwa nyuma yake; lakini wema ni kwa kumcha Allaah.”[5]

Kukiwekea kitendo nia kunakuwa katika yale mambo yaliyoamrishwa, na si katika yale yaliyoibahiswa au kukatazwa[6]. Kitu ambacho kinatilia nguvu maoni haya ni kwamba nadhiri juu ya mambo yaliyoibahishwa, yanayochukiza na yaliyoharamishwa hailazimiki kuitekeleza. Ikiwa mtu ataweka nadhiri ya kitu kilichoibahishwa, kinachochukiza au kilichoharamishwa basi haitomlazimu kuitekeleza tofauti na inavyomlazimu kumtii Allaah pale anapotia nadhiri ya kumtii. Bali ikiwa hakutimiza nadhiri yake basi itamlazimu kutoa kafara ya kiapo, kwa mujibu wa Ahmad na wengineo, ilihali wengine wanaona kuwa hakuna kinachomlazimu asipotekeleza nadhiri yake. Nadhiri haiwezi kugeuka ikawa kitu ambacho kikawaida sio utiifu wala ´ibaadah kwenda katika utiifu na ´ibaadah[7].

[1] al-Bukhaariy (56).

[2] Muslim (1006).

[3] Tazama ”adh-Dhakhiyrah” (1/239) ya al-Qaraafiy.

[4] Sharh Mukhtaswar Khaliyl (1/232).

[5] 2:189

[6] Tazama ”Ahkaam-ul-Qur-aan” (1/10) ya Ibn-ul-´Arabiy .

[7] Tazama ”Majmuu´-ul-Fataawaa” (11/450-451) ya IbnTaymiyyah.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 85-86
  • Imechapishwa: 29/05/2023