Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuhusu vita, Sunnah ni kupambana kwa kushusha sauti chini… Sauti za kwato za farasiwanaoenda mbio na ala za upepo, ambazo zinafanana na pembe ya mayahudi na kengele ya manaswara, hazikuwa zinatambulika katika zama za makhaliyfah waongofu wala viongozi wa waislamu waliokuja baada yao. Kutokana na ninavyodhania ni kwamba zilizuka kutoka kwa baadhi ya wafalme wa mashariki wa kifursi. Walizusha mambo mengi yenye kufungamana na uongozi na vita. Walipata uimara ulimwenguni kutokana na kwamba ufalme wao ulienea. Hatimaye matukio hayo yalienea kizazi kimoja baada ya kingine. Watu wakakulia hawajui kitu kingine zaidi yake. Bali waliwasimanga wale wenye kuwasema vibaya. Baadhi walifikia kudhani kwamba mambo hayo yametoka kwa ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh), ilihali mambo sivyo. Bali hayo hayakufanywa hata na makhaliyfah na viongozi wengine baada ya ´Uthmaan. Bali katika ummah kulidhihiri yale aliyosimulia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mtashika nyayo za nyumati zilizokuwa kabla yenu, shibiri kwa shibiri, dhiraa kwa dhiraa.” Wakasema: “ Wafursi na warumi?” Akasema: “Ni kina nani wengine kama si wao?”

Imekuja katika Hadiyth nyingine:

“Hakika mtafuata nyayo za wale waliokuwa kabla yenu hatua kwa hatua, shibiri kwa shibiri, mpaka wakiingia shimo la mburukenge nanyi mtaingia. Wakasema: “E Mtume wa Allaah! Unamaanisha mayahudi na manaswara?” Akasema: “Kina nani wengine?”[1]

Hadiyth zote mbili ni Swahiyh na zote zinafahamisha kuwa watapatikana baadhi ya watu watakaojifananisha na mayahudi na manaswara na watapatikana wengine ambao watajifananisha na wafursi na warumi. Kwa ajili hiyo kati ya askari wanaopigana vita kulionekana nembo za wa wafursi na watu wengine wenye kutoka nje, kukiwemokatika mavazi, mbuni za kivita na vyeo.

Kisha Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) akasema:

“Kinachokusudiwa hapa ni hizi sauti zilizozuliwa katika jambo la jihaad. Hata kama itadhaniwa kuwa kuna manufaa yenye nguvu, manufaa yenye nguvu yanapatikana kwa kulazimiana na mema yanayotambulika, kama ilivyo katika sauti za Dhikr. Wale waliotangulia kabla na wale waliowafata kwa wema ni wabora kuliko wale waliokuja nyuma katika kila jambo; katika swalah, Dhikr, kisomo cha Qur-aan, kusikiliza Qur-aan na mengineyo kama vile Jihaad, uongozi na mengine yanayohusiana nayo ya siasa, adhabu na ya kiuchumi. Mfumo wa Salaf ni kamilifu zaidi katika kila kitu, lakini muislamu anatakiwa kufanya katika hayo kwa kiasi anachoweza.”[2]

[1] al-Bukhaariy (4356) na Muslim (2669).

[2] al-Istiqaamah (1/324-331).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 83-85
  • Imechapishwa: 29/05/2023