57. Mifumo ya vita iliyoharamishwa

2 – Hoja tata nyingine ambayo inaweza kutumiwa, ni lile tukio linalohusiana na pale ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiga kambi karibu na maji yaliyoko Badr na al-Habbaab bin al-Mundhir bin ´Amr bin al-Jamuuh akamwambia:

“Ee Mtume wa Allaah, Allaah ndiye amekuweka mahali hapa ambapo hatutakiwi kusogeza kambi mbele au kuirudisha nyuma, au ni jambo linatokana na mtazamo, vita na njama?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ni jambo la mtazamo, vita na njama.” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Mahali hapa si pazuri. Andamana nasi katika ule upande wa maji yaliyoko karibu na watu ili badala yake tupige kambi hapo… Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapendezwa na maoni hayo na akaandamana nao.

Wanajengea dalili kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaacha Maswahabah wao ndio waamue mahali pa kupiga kambi na wakabainisha kuwa maeneo hayo hayakutengwa kwa mtazamo wa  Shari´ah, bali inahusiana na suala la kivita na njama. Kwa msemo mwingine, watu wanaoeneza shubuha hii, wanaona kuwa si lazima mfumo wa ulinganizi uafikiane na Qur-aan na Sunnah.

Mosi ni kwamba tukio hili halikuthibiti kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Imepokelewa na Ibn Ishaab ambaye amesema:

“Nimehadithiwa na kundi la watu kutoka Banuu Salamah ambao wamesimulia kuwa al-Habbaab… “[1]

Kama unavyoona cheni ya wapokezi wake ni dhaifu. al-Haakim ameipokea kwa cheni ya wapokezi ilioungana[2], lakini adh-Dhahabiy amesema:

“Hadiyth ni munkari na cheni ya wapokezi wake.”[3]

Namna hii ndivo ilivyokuja katika chapa. Muhaddith al-Albaaniy amesema:

“Huenda ilitakiwa iwe ´dhaifu` badala ya ´na cheni ya wapokezi wake`. Katika cheni ya wapokezi wake kuna watu nisiowajua.”[4]

Kadhalika imepokelewa na al-Bayhaqiy katika “ad-Dalaail” kwa cheni ya wapokezi dhaifu. Katika “al-Bidaayah” imetajwa kuwa al-Umawiy ameipokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas. Lakini kwenye cheni ya wapokezi wake kuna al-Kalbiy ambaye alikuwa mwongo.

Pili ni kwamba katika tukio hilo hakuna dalili waliyoishikilia. Kila mwenye akili anatambua ya kwamba kuchagua mahali pa kupiga kambi – kuanzia wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka siku ya Qiyaamah – si jambo linalotegemea Qur-aan na Sunnah. Bali hata haiwezi kufikiriwa kuwa linatokana na Qur-aan na Sunnah. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anaagiza viongozi wa vita, akiwafunza hukumu za jihaad na akiwanasihi pasi na kuwateulia mahali ambapo wanatakiwa kupiga kambi. Vivyo hivyo ndivo walivyokuwa wakifanya makhaliyfah wake waongofu. Kadhalika ndivyo ilivyokuwa pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anashika njia kwenda katika jihaad; walikuwa wanashika njia yoyote na si jambo limefungamana na hukumu ya Shari´ah.

Mfumo wa jihaad katika njia ya Allaah (Ta´ala) ni jambo linatakiwa kuafikiana na Qur-aan na Sunnah. Haijuzu kwa yeyote kuingiza ndani yake yale ambayo hayakuwa yakifanywa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah wake watukufu. Mwongozo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vitani ndio mwongozo mkamilifu zaidi. Hakuna kubwa wala dogo linalohusiana na jihaad, isipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuachia elimu yake. Mwenye kuijua, ameijua, na mwenye kuijahili, ameijahili. Kwa ajili hiyo Salaf walimfanyia ukali yule mwenye kuzua kitu katika mambo yanayohusiana na vita na jihaad ambayo hayakuwepo wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] as-Siyrah an-Nabawiyyah (2/272).

[2] al-Mustadrak (3/462-467).

[3] Talkhiysw-ul-Mustadrak (3/462-467).

[4] Maelezo ya ”Fiqh-us-Siyrah”, uk. 224.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 82-83
  • Imechapishwa: 29/05/2023