Kutokana na yaliyotangulia tunaweza kufupisha kwa kusema:

1 – Mifumo ya kulingania inatakiwa iafikiane na Qur-aan na Sunnah. Haijuzu kwa mtu anayemwamini Allaah na Siku ya mwisho kuzidisha katika ulinganizi kitu ambacho hakikufanywa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake watukufu. Hoja ya hilo ni kuenea kwa dalili zinazoonyesha kuwa dini imekamilika na kubainisha kila kitu kinachomfanya mtu kuwa karibu na Pepo na kumuweka mbali na Moto. Aidha hitimisho hii inatiliwa nguvu na ueneaji wa dalili zinazotahadharisha mambo yaliyozuliwa ndani ya dini na zinazoamrisha kushikamana na dini ya kwanza. Kwa ajili ya kuthibitisha usahihi wa dalili wa mada hiyo, nimenakili maneno ya wanazuoni kadhaa wahakiki ambao wamekataza waziwazi mifumo yote yenye kuzuliwa katika ulinganizi kwa kutegemea maandiko ya Qur-aan na Sunnah pamoja na maneno ya Salaf. Baadhi ya wanazuoni hao ni:

1 – Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah)

2 – Shaykh Hamuud at-Tuwayjiriy (RahimahuAllaah)

3 – Shaykh Bakr bin ´Abdillaah Abu Zayd (Rahimahu Allaah)

4 – Shaykh na ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz (Rahimahu Allaah)

5 – Imaam, ´Allaamah na Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn (Rahimahu Allaah)

Kitu cha ziada kinachoyapa nguvu maoni haya, ni ukali wa Salaf kukemea njia zote zilizozuliwa ijapo zitakuwa ni zenye kuilainisha mioyo, macho kutiririka machozi au – kama inavyosemwa leo – kunufaisha. Ni jambo linalotambulika vyema kwamba Salaf waliwakaripia wasimuliaji visa na waimbaji wanaoimba pasi na ala za muziki.

2 – Kuzua mfumo wa ulinganizi kunazingatiwa ni kuzua ndani ya dini na kuiacha njia ya waumini. Kuzua mifumo mipya ya ulinganizi ni jambo halikutambulika isipokuwa kwa watu wa matamamio Ahl-ul-Bid´ahna khaswa Suufiyyah; wao ndio watangulizi wa kuzua mifumo ya kisasa.

3 – Kujengea hoja kwa baadhi ya wajinga juu ya vyombo vya kiufundi vya kisasa ni jambo la batili na hoja yenye kurudishwa. Kitabu hiki kimebainisha kwamba hakuna kugongana kati ya kwamba mfumo wa ulinganizi ni lazima uwe kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah sambamba na hilo utumiaji wa vyombo hivyo, kwa sharti vyombo hivyo visiwe vimekatazwa kwa mujibu wa Shari´ah.

Namuomba Allaah (´Azza wa Jall) afanye kitabu hiki kiwe kimeandikwa kwa ajili Yake kwa lengo la kupata Pepo Yake iliyojaa neema na afanye manufaa yake ni yenye kuenea – hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuitikia na yukaribu. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 91-92
  • Imechapishwa: 30/05/2023