Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Himdi zote anastahiki Allaah. Mwisho mwema ni kwa wenye kumcha na hakuna uadui isipokuwa kwa madhalimu. Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika – Mungu wa wale wa mwanzo na wale wa mwisho na Mwenye kuzisimamia mbingu na ardhi – na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja, Mtume Wake na kipenzi chake mwandani na mwaminifu juu ya Wahy Wake. Amemtumiliza kwa watu wote hali ya kuwa ni mwenye kutoa bishara njema na mwenye kuonya na mwenye kulingania katika dini ya Allaah kwa idhini Yake na hali ya kuwa ni taa lenye kuangaza – swalah na amani ziwe juu yake, kizazi chake na Maswahabah zake ambao wamepita juu ya njia yake katika kulingania katika njia Yake, wakasubiri juu ya hilo na wakapambana ndani yake mpaka Allaah alipoishindisha dini Yake kupitia wao, akalinyanyua neno lake ijapo watachukia washirikina – amsalimishe salamu nyingi.

Ama baada ya hayo;

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewaumba viumbe ambao ni watu na majini ili wamwabudu Yeye pekee asiyekuwa na mshirika, watukuze amri na makatazo Yake na atambulikekwa majina na sifa Zake. Amesema (´Azza wa Jall):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.”[1]

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu ambae amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kumcha Allaah.”[2]

اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ وَمِنَ الْأَرْضِ مِثْلَهُنَّ يَتَنَزَّلُ الْأَمْرُ بَيْنَهُنَّ لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

”Allaah ndiye ambaye ameziumba mbingu saba na katika ardhi mfano wa hizo, inateremka amri kati yao ili mjue kwamba Allaah juu ya jambo ni Muweza na kwamba Allaah amekizunguka kila kitu kwa Ujuzi.”[3]

Akabainisha (Subhaanah) kwamba amewaumba viumbe ili wamwabudu, wamtukuze na watii amri na makatazo Yake. Kwa sababu ´ibaadah ni kule kumpwekesha na kumtii hali ya kutukuza maamrisho na makatazo Yake. Aidha akabainisha (Subhaanah) ya kwamba ameziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ili atambulike kuwa Yeye juu ya kila jambo ni muweza na kwamba amekizunguka kila kitu kwa utambuzi. Kupitia hayo ikatambulika kuwa hekima ya kuumbwa viumbe ni Allaah kutambulika kwa majina na sifa Zake, kwamba juu ya kila jambo ni muweza na ni mtambuzi wa kila kitu (Jalla wa ´Alaa). Hiyo pia ndio hekima ya kuumbwa kwa Mitume na kuteremshwa kwa Vitabu. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.””[4]

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[5]

لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ

“Kwa hakika Tuliwapeleka Mitume Wetu kwa hoja za wazi na tukateremsha pamoja nao Kitabu na Mizani ili watu wasimamie kwa uadilifu.”[6]

كَانَ النَّاسُ أُمَّةً وَاحِدَةً فَبَعَثَ اللَّـهُ النَّبِيِّينَ مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ وَأَنزَلَ مَعَهُمُ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِيَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ فِيمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ

“Watu walikuwa ummah mmoja kisha Allaah akawatuma Mitume hali ya kuwa ni wabashiriaji na waonyaji na Akateremsha pamoja nao Kitabu kwa haki ili kihukumu kati ya watu katika ambayo wamekhitilafiana kwayo.”[7]

Akabainisha (Subhaanah) ya kwamba amewatuma Mitume na akateremsha vitabu ili wahukumu kati ya watu kwa haki na kwa uadilifu na wawawekee wazi yale mambo ya Shari´ah na I´tiqaad waliyokhtilafiana kwayo. Aidha mambo ya Tawhiyd. Amesema (Subhaanah):

كَانَ النَّاسُ أُمَّةً وَاحِدَةً

“Watu walikuwa ummah mmoja… ”

Bi maana juu ya haki.

Kuanzia wakati wa Aadam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka wakati wa Nuuh hawakutofautiana. Watu walikuwa juu ya uongofu. Hivo ndivo alivosema Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) na jopo katika watu wa kale na waliokuja baadaye. Halafu ikatokea shirki kwa watu wa Nuuh ambapo wakatofautiana kati yao na wakatofautiana katika yanayowalazimu kuhusu haki ya Allaah. Wakati kulitokea shirki na tofauti ndipo Allaaha kamtumiliza Nuuh (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Mitume wengine baada yake. Amesema (´Azza wa Jall):

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ

“Hakika Tumekufunulia Wahy kama tumevyomfunulia Wahy Nuuh na Manabii baada yake.”[8]

وَمَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ إِلَّا لِتُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي اخْتَلَفُوا فِيهِ ۙ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

”Hatukukuteremshia Kitabu isipokuwa ili uwabainishie yale waliyokhitilafiana kwayo na pia iwe ni mwongozo na Rahmah kwa watu wanaoamini.”[9]

Allaah ameteremsha kitabu ili kihukumukatika yale ambayo watu wametofautiana, abainishe Shari´ah Yake katika yale ambayo watu wameyajahili, awaamrishe watu kulazimiana na Shari´ah Yake, kusimama kwenye mipaka Yake na awakataze watu kutokamana na yale yanayowadhuru duniani na Aakhirah.

[1] 51:56

[2] 02:21

[3] 65:12

[4] 16:36

[5] 21:25

[6] 57:25

[7] 02:213

[8] 04:163

[9] 16:64

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 03-07
  • Imechapishwa: 30/05/2023