Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) wamemaliziwa kwa ambaye ni mbora na kiongozi wao, bwana wao, Mtume wetu na kiongozi wetu Muhammad bin ´Abdillaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amefikisha ujumbe, akatekeleza amana, akaunasihi Ummah, akapambana jihaad katika njia ya Allaah ukweli wa kupambana, akalingania kwa Allaah kwa siri na kwa dhahiri na akaudhiwa maudhi makubwa. Hata hivyo alisubiri juu ya hayo kama walivyosubiri Mitume wengine (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Alisubiri kama walivyosubiri na alifikisha kama walivyofikisha. Lakini alifanyiwa maudhi zaidi, akasubiri zaidi na akatekeleza Ujumbe kwa njia kamili zaidi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aliishi miaka ishirini na tatu akifikisha ujumbe wa Allaah, akilingania kwayo na akieneza hukumu zake. Katika miaka hiyo miaka kumi na tatu alikuwa Makkah akiwalingania watu kwa siri. Baadaye akafanya hivo hadharani. Alitangaza haki, akaudhiwa, akasubiri juu yaulinganizi na maudhi ya watu licha ya kuwa wanajua ukweli na amana yake. Vilevile wanajua utukufu, nasaba yake na nafasi yake. Lakini inahusiana na matamanio, ukaidi unaotoka kwa watukufu, ujinga na watu wa kawaida kufuatakichwa mchunga. Wale wakuu walipinga, wakafanya kiburi, wakakanusha, wakafanya jeuri na husuda. Watu wa kawaida waliigiliza, wakafuata na wakafanya vibaya. Matokeo yake akaudhiwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) maudhi makubwa. Yanayojulisha kwamba wakuu walitambua haki lakini hata hivyo wakafanya ukaidi ni maneno Yake (Subhaanah):

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Hakika tunajua kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Hakika wao hawakukadhibishi wewe lakini madhalimu wanakanusha alama za Allaah.”[1]

Akabainisha (Subhaanah) ya kwamba hawamkadhibishi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bali wanatambua ukweli na uaminifu wake juu ya batili. Walikuwa wakimwita mwaminifu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kabla ya kuanza kuteremshiwa Wahy. Lakini walipinga haki hali ya kuwa na husuda na chuki (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini hata hivyo yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakujali jambo hilo na wala hakulitambua. Alifanya subira, akataraji malipo kutoka kwa Allaah na akaendelea juu ya njia yake. Aliendelea kulingania katika dini ya Allaah (Jalla wa ´Alaa), hali ya kusubiri juu ya maudhi, mpambanaji katika kulingania, akijizuilia kuwaudhi wengine,akivumulia maudhi anayofanyiwa, akiyachukulia poa yale yanayotoka kwao kwa kiasi inavyowezekana. Hali iliendelea hivo mpaka ukapamba moto na wakaazimia kumuua (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hapo ndipo Allaah akampa idhini ya kutoka kwenda Madiynah. Akahamia huko (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ikawa ndio mji mkuu wa kwanza wa Uislamu. Dini ya Allaah ikadhihiri na waislamu wakawa na dola yenye nguvu. Akaendelea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kulingania na kuiweka wazi haki. Akaanzisha jihaad kwa silaha na akawatumiliza Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) wakiwalingania watu katika kheri na uongofu na wanawapambanulia ulinganizi wa Mtume wao Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akatuma vikosi na akapambana vita vinavotambulika mpaka pale Allaah aliposhindisha dini yake kupitia mikono yake, Allaah akakamilisha dini kupitia kwake, akamtimizia neema yeye na Ummah wake. Akafa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya Allaah kumkamilishia dini yake na kufikisha ufikishaji wa wazi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 06:33

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 07-10
  • Imechapishwa: 30/05/2023