Kuswalishwa na imamu anayeswali swalah nyingine

Je, ni sharti aina ya swalah ya imamu iafikiane na ya maamuma? Bi maana Dhuhr nyuma ya anayeswali Dhuhr, ´Aswr na ´Aswr na kadhalika? Hili lina tofauti:

1 – Kuna wanachuoni waliosema kuwa ni wajibu swalah mbili ziafikiane. Mtu aswali Dhuhr nyuma ya anayeswali Dhuhr, ´Aswr nyuma ya anayeswali ´Aswr, Maghrib nyuma ya anayeswali Maghrib, ´Ishaa nyuma ya anayeswali ´Ishaa na Fajr nyuma ya anayeswali Fajr.  Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imamu amewekwa ili afuatwe. Hivyo basi, msiende kinyume naye.”[1]

2 – Wanachuoni wengine wakasema kuwa haikushurutishwa. Inajuzu kuswali ´Aswr nyuma ya anayeswali Dhuhr, Dhuhr nyuma ya anayeswali ´Aswr na ´Aswr nyuma ya anayeswali ´Ishaa. Umaamuma katika hali hauathiri. Ikiwa inajuzu kuswali faradhi nyuma ya anayeswali swalah inayopendeza, pamoja na kuwa ni hukumu tofauti, vilevile tofauti ya jina haidhuru. Maoni haya ndio sahihi zaidi.

Mtu akiuliza; wakati kumepokimiwa swalah ya ´Ishaa na kutaka kuswali nimekumbuka kuwa niliswali Dhuhr pasina wudhuu’. Vipi nitaswali Dhuhr nyuma ya anayeswali ´Ishaa? Tunasema jiunge na imamu na uswali Dhuhr. Wewe nia yako ni Dhuhr na imamu nia yake ni ´Ishaa. Hili halidhuru.

“Hakika si venginevyo kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kwa kile alichonuia.”

Kuhusiana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Imamu amewekwa ili afuatwe. Hivyo basi, msiende kinyume naye.”

haina maana kutotofautiana naye katika nia. Kwa sababu alifafanua na kuweka wazi kwa kusema:

“Akisema “Allaahu Akbar” nanyi semeni “Allaahu Akbar”, akisujudu nanyi sujudini, akipanda juu nanyi pandeni juu.”

Bi maana mfuateni na msimtangulie. Maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baadhi yanafasiri mengine.

[1]al-Bukhaariy (689).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (01/385-386)
  • Imechapishwa: 30/05/2023