59. Wakati ambapo sijda ya kusahau inakuwa kabla na baada ya salamu

Swali 59: Baadhi ya maimamu wanaleta Sujuud ya kusahau baada ya salamu, baadhi ya wengine wanaleta Sujuud ya kusahua kabla ya salamu na wako ambao wanasujudu mara kabla ya salamu na mara baada ya salamu. Ni lini imesuniwa kusujudu kabla ya salamu na ni lini imesuniwa baada yake? Yale yaliyosuniwa kuleta Sujuud kabla ya salamu au baada yake ni kwa njia ya ulazima au njia ya kupendeza tu?

Jibu: Wigo ni mpana wa suala hili. Yote mawili yanafaa; kusujudu kabla ya salamu na baada yake. Kumepokelewa Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya yote mawili. Lakini bora Sujuud ya kusahau iwe kabla ya salamu. Isipokuwa katika sura mbili:

1 – Akimaliza swalah kwa kupunguza Rak´ah isiyopungua moja. Katika hali hii Sujuud ya kusahau iletwe baada ya kukamilisha swalah na kutoa salamu kwa ajili ya kumwigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika jambo hilo. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipotoa salamu kwa kupunguza Rak´ah mbili katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) na kwa kupunguza Rak´ah moja katika Hadiyth ya ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anhumaa), alisujudu Sujuud ya kusahau baada ya kukamilisha na kutoa salamu.

2 – Akiingiwa na shaka ndani ya swalah yake na asijue ni Rak´ah ngapi ameswali; tatu au nne katika swalah za Rak´ah nne, au Rak´ah mbili au tatu katika Maghrib, au Rak´ah moja au mbili katika Fajr, hata hivyo akawa na dhana yenye nguvu ya moja kati ya mambo hayo mawili, dhana kubwa yenyewe ni kama amepunguza au ameswali kikamilifu, basi anatakiwa kujengea juu ya kile ambacho inampelekea dhana yake kubwa na Sujuud yake iwe baada ya salamu. Hapa ni kwa njia ya ubora. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Ibn Mas´uud iliyotajwa katika jawabu la 58.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 63
  • Imechapishwa: 07/09/2022