58. Mswaliji afanye nini akiingiwa na shaka ya Rak´ah alizoswali?

Swali 58: Mswaliji afanye nini akiingiwa na shaka kama ameswali Rak´ah tatu au nne?

Jibu: Kinachompasa akiingiwa na shaka basi ajengee juu ya yakini ambayo ni ile idadi ya chini. Hivo ni kufanya kuwa ameswali Rak´ah tatu kutokana na sura iliyotajwa na baada ya hapo aswali Rak´ah ya nne kisha alete Sujuud ya kusahau na atoe Tasliym. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakapokuwa na shaka mmoja wenu katika swalah yake na asijue [ni Rak´ah] ngapi ameswali, tatu au nne, basi atupilie mbali ile shaka na ajengee kwa lile aliloyakinisha katika moyo wake kisha asujudu Sujuud mbili kabla ya kutoa salamu. Ikiwa atakuwa ameswali Rak´ah tano, basi swalah yake itamfanyia uombezi. Na ikiwa atakuwa ameswali swalah kikamilifu nne, basi hio itakuwa ni fedheha kwa shaytwaan.”

Ameipokea Imaam Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh).

Lakini akiwa na dhana kubwa ya moja kati ya mambo mawili kati ya kupunguza au kukamilisha, basi ajengee juu ya kile ambacho dhana yake kubwa inampelekea kisha atoe Tasliym halafu asujudu Sujuud mbili baada ya kutoa Tasliym. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakapokuwa na shaka mmoja wenu katika swalah yake, basi ajitahidi lililo la sawa na aendelee kwa hilo. Baadaye atoe salamu kisha asujudu sijda mbili baada ya salamu.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 07/09/2022