Baadhi ya ndugu waheshimiwa wameniuliza maoni yangu kuhusu uchaguzi. Maoni yangu mpaka hivi sasa naona kuwa kimsingi ni kwamba uchaguzi sio jambo la Kiislamu. Hata hivyo wako baadhi ya wanazuoni – ambao ni wabora na wajuzi zaidi kuliko mimi – wametoa fatwa za kujuzisha uchaguzi wakati kunapokuwa kuna dharurah kubwa kwa kutimia sharti kadhaa. Moja katika sharti hizo ni mtu awe na dhamana, au angalau kwa uchache dhana kubwa, kwamba yule mgombea atakayeshinda atahukumu kwa Shari´ah ya Allaah, atasimamisha adhabu za ki-Shari´ah na dini. Ni ipi hukumu ambaye anafanyia kazi fatwa hii? Je, inafaa kumuona kuwa ni mzushi?

Hapana, haijuzu kumzingatia kuwa ni mzushi, wala kumlazimisha maoni mengine, muda kuwa ametegemea fatwa ya wanazuoni ambao wanaona msimamo huu ambao pengine mimi naona kinyume chake. Mimi sifanyii ushabiki maoni yangu na wala siwalazimishi watu maoni yangu – lakini nashikilia maoni yangu ninayoona kuwa ndio ya sawa juu ya masuala haya.

Ama yale yanayofanywa na vijana wajinga ambapo wanatiana katika Bid´ah kwa sababu ya masuala haya, ninawaambia wamche Allaah. Badala yake kusanyikeni juu ya Qur-aan na Sunnah na jitahidini katika kufikia Shari´ah ya Kiislamu, ni mamoja mko Libya au nchi nyingine. Msijishughulishe kutiana katika Bid´ah, ukafiri au dhambi kwa sababu ya jambo hili. Pengine wakati mtu atakuwa na dhana yenye nguvu na nia njema ikawa suala hili linaingia katika yale masuala ya kujitahidi.

Nataraji ujumbe huu utawafikia ndugu wote katika kila mahali katika nchi za Kiislamu ambazo zinasumbuliwa na fitina hii, wajitahidi kuwa na umoja juu ya Qur-aan na Sunnah na wasambae kila mahali kiasi cha kwamba kusiweko kingine kinachohukumiwa isipokuwa kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah (´Azza wa Jall) maneno, matendo, ´Aqiydah, kusimamisha adhabu, adabu, tabia, ´ibaadah na mwenendo, ili watoke katika majanga haya ambayo wanaishi ndani yake.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin Sa´d as-Suhaymiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.youtube.com/watch?app=desktop&v=bYOyeSjZqkM
  • Imechapishwa: 07/09/2022