56. Ana mazowea ya kulipa Ramadhaan katika miji ya kikafiri

Swali 56: Je, anapata dhambi ambaye amezowea kulipa Ramadhaan katika nchi isiyokuwa ya Kiislamu[1]?

Jibu: Hapa kunahitajika maelezo. Muislamu anafurahi kwa kufika kwa Ramadhaan na anafurahishwa imfikie hali ya kuwa katika nchi ya Kiislamu. Hilo ni kutokana na zile nembo zinazopatikana katika Ramadhaan kwa yule aliyeko katika mji wa Kiislamu, ambazo hawezi kuzihisi yule ambaye yuko nje ya mji usiokuwa wa Kiislamu. Kwa mfano anawaona waswaliji, wingi wao na kushindana kwao katika matendo mema, jambo ambalo linamzidishia uchangamfu, nguvu na shauku ya kheri.

Ambaye yuko katika nchi isiyokuwa ya Kiislamu, basi yumo khatarini ya kupungua thawabu zake kutokana na uchache wa matendo yake mema au akapata dhambi kwa sababu ya kutenda kwake dhambi. Pengine madhambi yake yakaongezeka kwa sababu ya kuwa kwake mbali na watu wa kheri na kuwa kwake karibu na waovu.

Ni lazima kwa ambaye amezowea kufanya hivo kumcha Allaah, aache tabia hiyo na afunge Ramadhaan katika mji wa Kiislamu. Lakini ikiwa kufunga kwake katika mji  usiokuwa wa Kiislamu kutokana na kitendo kinachokubalika katika Shari´ah, kama mfano wa kuwalingania kwa Allaah, kuwaswalisha waislamu katika zile swalah tano na mengineyo katika matendo ya kheri, basi hayo ni katika yale ambayo muislamu anapewa ujira na thawabu kwayo. Pengine kwa kufanya kwake hivo akapata thwabu ambazo hawezi kuzipata anapokuwa katika mji usiokuwa wa Kiislamu kutokana na ile kazi anayofanya ambayo ni kuwalingania watu kwa Allaah, kuwafunza watu kheri pamoja na kujichunga na kila shari.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (15/329-330).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 78-79
  • Imechapishwa: 22/05/2022