Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Muumbaji wa vitu hivi ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa.”

MAELEZO

Wakati Shaykh alipobainisha kuwa Mola ndiye mwabudiwa na akatumia dalili kwa maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Ambae amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na ucha Mungu.”

Akatumia ushahidi kwa maneno ya Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) katika tafsiri yake juu ya Aayah na akataka kubainisha aina za ´ibaadah na dalili ya kila aina. ´Ibaadah kilugha maana yake ni kujidhalilisha na kunyenyekea. Kunasemwa طريق معبد ikiwa na maana kwamba imedhalilishwa na kunyenyekezwa ili kutembelea juu yake.

´Ibaadah imegawanyika aina mbili:

1- ´Ibaadah yenye kuenea kwa watu wote. Wote ni waja wa Allaah. Waumini na makafiri, watenda madhambi na wanafiki. Wote hawa ni waja wa Allaah. Hiyo ina maana kwamba wako chini ya uendeshaji na nguvu Zake na kwamba ni lazima kwao kumwabudu Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Hii ni ´ibaadah yenye kuwaenea watu wote kuanzia waumini mpaka makafiri. Wote hawa ni waja wa Allaah. Kwa msemo mwingine ni kwamba wameumbwa kwa ajili Yake na ni wenye kudhalilishwa. Hakuna yeyote katika wao anayetoka nje ya mshiko na ufalme Wake. Amesema (Ta´ala):

إِن كُلُّ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِلَّا آتِي الرَّحْمَـٰنِ عَبْدًا

“Hakuna yeyote yule aliyeko katika mbingu na ardhi isipokuwa atamjia ar-Rahmaan, hali ya kuwa ni mja.”[1]

Hapa wanaingia wale wote walioko mbinguni na ardhini, waumini na makafiri. Wote watakuja siku ya Qiyaamah hali ya kuwa ni wenye kunyenyekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna yeyote katika wao ana ushirika pamoja na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) katika ufalme Wake.

2- ´Ibaadah maalum kwa waumini. Amesema (Ta´ala):

وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا

“Na waja wa ar-Rahmaan ni wale wanaotembea juu ya ardhi kwa unyenyekevu na upole.”[2]

إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ

”Hakika waja wangu huna mamlaka nao.”[3]

إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ

“Isipokuwa waja Wako katika wale walioteuliwa kwa ikhlaasw.”[4]

 Huu ni uja maalum. Ni ule uja wa utiifu na kujikurubisha kwa Allaah kwa Tawhiyd.

[1] 19:93

[2] 25:63

[3] 15:42

[4] 15:40

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 121-122
  • Imechapishwa: 22/12/2020