Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mola ndiye Mwabudiwa. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Ambae amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na ucha Mungu. Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa na akateremsha kutoka mbinguni maji, akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Hivyo basi msimfanyie Allaah washirika na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”[1]

MAELEZO

Mola ndiye mwabudiwa – Bi maana ndiye ambaye anastahiki kuabudiwa. Wengine hawastahiki kuabudiwa kwa sababu sio waola. Haya ndio makusudio ya maneno ya Shaykh (Rahimahu Allaah) pale aliposema:

“Mola ndiye mwabudiwa.”

Bi maana ndiye anayestahiki kuabudiwa. Jengine ni kwamba haitoshi kwamba mtu anakubali uola wa Allaah. Bali ni lazima kukubali pia ´ibaadah kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na aifanye hali ya kumtakasia Yeye nia. Muda wa kuwa umekubali kwamba Yeye ndiye Mola basi imekulazimu ukubali kwamba Yeye ndiye mwenye kuabudiwa na kwamba wengineo hawastahiki kitu katika ´ibaadah. Dalili juu ya kwamba ´ibaadah ni maalum kwa Mola ni maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Ambae amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na ucha Mungu. Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa na akateremsha kutoka mbinguni maji, akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Hivyo basi msimfanyie Allaah washirika na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”

Enyi watu – Hapa Allaah anawaita watu wote; waumini na makafiri. Kwa sababu ametaja katika Suurah hii “al-Baqarah” kugawanyika kwa watu mafungu matatu:

1- Waumini ambao wanaamini mambo yaliyojifichikana, wanaamini siku ya Mwisho na akawasifia kwamba wao ndio wenye kufaulu pale aliposema:

أُولَـٰئِكَ عَلَىٰ هُدًى مِّن رَّبِّهِمْ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Hao wako juu ya uongofu kutoka kwa Mola wao na hao ndio wenye kufaulu.”[2]

2- Makafiri waliodhihirisha ukafiri na ukaidi. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا سَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَأَنذَرْتَهُمْ أَمْ لَمْ تُنذِرْهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ

“Hakika wale waliokufuru ni mamoja kwao ukiwaonya au usiwaonye, wao hawatoamini.”[3]

3- Wanafiki ambao hawako pamoja na makafiri na wala hawako pamoja na waumini:

مُّذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذَٰلِكَ لَا إِلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ وَلَا إِلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ

“Wanayumbayumba baina ya hayo [imani na ukafrii]; huku hawako wala huko hawako.”[4]

Ni waumini kwa nje lakini ni makafiri kwa ndani. Hawa ni waovu zaidi kuliko makafiri wenye kuonyesha waziwazi ukafiri wao. Ndio maana wao wakateremshiwa Aayah kumi na zaidi ilihali waumini wameteremshiwa Aayah chache na makafiri Aayah mbili. Kuhusu wanafiki ameanza kuwataja pale aliposema:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ

“Miongoni mwa watu wako wasemao “Tumemuamini Allaah na siku ya Mwisho hali ya kuwa si wenye kuamini.”[5]

Mpaka pale aliposema:

يَكَادُ الْبَرْقُ يَخْطَفُ أَبْصَارَهُمْ

“Unakaribia umeme kunyakua macho yao.”[6]

Yote haya ni kwa wanafiki kutokana na ukubwa wa khatari yao na ubaya wa matendo yao. Pindi alipotaja aina tatu za watu hawa akasema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ

“Enyi watu!”

Huu ni wito kwa watu aina zote hizi waumini, makafiri na wanafiki. Wanachuoni wamesema:

“Mwito wa kwanza ndani ya msahafu ni huu:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu… “

Mwabuduni – Kitendo cha amri. Maana yake mtakasieni Yeye ´ibaadah. Kwa nini? Kwa sababu Yeye ndiye Mola wenu. ´Ibaadah haisilihi isipokuwa kwa Mola (Subhaanahu wa Ta´ala). Kisha akataja dalili ya hilo ambayo ni maneno Yake:

الَّذِي خَلَقَكُمْ َ

“… ambae amekuumbeni… ”

وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ

“… na wale wa kabla yenu… “

Nyumati zote. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewaumba Malaika, majini na watu na viumbe wengine wote.

لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“… mpate kuwa na ucha Mungu.”

Mkiyazingatia haya basi huenda yakakusababishieni uchaji Allaah. Mkizingatia kwamba Yeye ndiye kakuumbeni na kawaumba wale wa kabla yenu basi huenda mkamcha Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) wakati wa kumwabudu. Kwa sababu hakuna kitu kinachosalimisha kutokamana na adhabu Yake isipokuwa kumtii Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Huenda mkaogopa adhabu Yangu na mkaogopa Moto. Kwa sababu hakuna kitu kitachowasalimisheni isipokuwa kumwabudu Mola wenu ambaye amekuumbeni na akawaumba wale wa kabla yenu. Kisha akaendelea kuonyesha dalili juu ya uola na ´ibaadah Yake (Subhaanahu wa Ta´ala) pale aliposema:

جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا

“Ambaye amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko.”

Bi maana busati:

وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ بِسَاطًا

”Allaah amekufanyieni ardhi kuwa kama busati.”[7]

Busati na tandiko kwa maana nyingine mnalala juu yake, mnalima juu ya mgongo wake, mnapita juu yake wakati wa safari zenu popote mnapotaka. Ardhi ni tandiko na imetandazwa:

وَالْأَرْضَ فَرَشْنَاهَا فَنِعْمَ الْمَاهِدُونَ

“Na ardhi Tumeitandaza – basi uzuri ulioje wa Wenye kutayarisha!”[8]

Kwa ajili ya manufaa yenu.

وَالسَّمَاءَ بِنَاءً

”… na mbingu kuwa ni paa.”

Mbingu ndio paa ya ardhi na ndani yake kuna manufaa kwa waja:

وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ

“… akateremsha kutoka mbinguni maji, akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Hivyo basi msimfanyie Allaah washirika na hali ya kuwa nyinyi mnajua.”

[1] 02:21-22

[2] 02:05

[3] 02:06

[4] 04:143

[5] 02:08

[6] 02:20

[7] 71:19

[8] 51:48

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 118-121
  • Imechapishwa: 22/12/2020