1- al-Husayn bin Fahm amesema:

“Nimemsikia Yahyaa bin Ma´iyn akisema: “Nilikuwa Misri pindi nilipomuona kijakazi mmoja akiuzwa kwa dinari elfu. Sijapatapo kumuona mwanamke mrembo kama yeye. Allaah amswalie.” Ndipo nikasema: “Ee Abu Zakariyyaa! Hivi kweli mtu kama wewe unasema hivo?” Akasema: “Ndio. Allaah amswalie yeye na kila mwanamke mrembo.”[1]

2- Swaalih bin Ahmad bin Hanbal amesema:

“Baba yangu alinambia: “Mama yako alikuwa akishona vitambara na akiuza mapazia kwa ajili ya kupata vijisarafu vya fedha. Hilo ndilo lilikuwa pato letu.”[2]

3- Swaalih bin Ahmad bin Hanbal amesema:

“Ilikuwa wakati mwingine inaweza kutokea tukanunua kitu na kukizuia kwa ajili yake ili asije kutukaripia.”[3]

4- al-Murruudhiy amesema:

“Nilimsikia Abu ´Abdillaah akimtaja mke wake, akimuomba Allaah amrehemu na akisema: “Tuliishi pamoja kwa miaka ishirini na hakuwahi kamwe kutofautiana juu ya neno hata moja.” Hatujui kama Ahmad alioa mke wa tatu.”

5- Ya´quub bin Bukhtaan amesema:

“Abu ´Abdillaah alituamrisha kumnunulia mjakazi. Akatuwahi njiani mimi na Fawraan akasema: “Ee Abu Yuusuf! Mwanamke huyo awe amejazajaza.”

6- al-Marruudhiy amesema:

“Siku mbili kabla ya kufariki kwa Ahmad alisema kwa sauti nyonge: “Niitieni watoto wote.” Watoto wote wakakusanyika na akaanza kuwanusa na kuwapapasa juu ya vichwa vyao. Macho yake yalikuwa yamejawa na machozi. Nikaweka beseni chini yake na nikaona mkojo wake ulikuwa ni damu. Nikamweleza daktari ambapo akasema: “Mtu huyu huzuni na masikitiko yamevunja undani wake.”[4]

7- Ibn Abiy Haatim amesema:

“al-Hasan bin ´Arafah aliishi miaka 110. Aliruzukiwa watoto kumi na wote aliwapa majina ya wale Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) kumi waliobashiriwa Pepo.”[5]

[1] Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (11/87)

[2] Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (11/324).

[3] Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (11/334).

[4] Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (11/336).

[5] Siyar A´laam-in-Nubalaa’ (11/549).

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’
  • Imechapishwa: 22/12/2020