54. Hoja tata ya kwanza kuhusu mfumo wa kulingania uliozuliwa

1 – Kuna hoja tata zinazotumiwa na wale watu ambao wanaona kuwa mifumo ya ulinganizi si lazima iafikiane na Qur-aan na Sunnah. Hoja tata ya kwanza, inayohusiana na nyimbo, imetajwa na Abul-Qaasim al-Qushayriy na baadaye ikaraddiwa na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake “al-Istiqaamah”. Nitataja maneno ya al-Qushayriy kisha baadaye nitatajakwa ufupi maneno ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah akimraddi, kwa sababu maneno yake ni mazuri na yenye kubainisha katika masuala haya. Abul-Qaasim al-Qushayriy amesema:

“Kwa ujumla inafaa kusikiliza mashairi yanayosomwa kwa melodina toni zenye ladha, ikiwa yule msikilizaji haitakidi jambo la haramu, hasikilizi kitu kilichosimangwa na dini wala hakutumbukia katika matamanio yaliyokatazwa wala pumbao. Hapana shaka yoyote kwamba mashairi yalisomwa mbele yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala hakuwakaripia. Ikijuzu kuyasikiliza pasi namelodi, basi kilicho dhahiri ni kwamba hukumu haibadiliki kwa kuyasikiliza kwamelodi. Isitoshe zingatia kuwa yale yanayompelekea msikilizaji kuwa na shauku ya utiifu, kukumbuka yale ambayo Allaah amewaandalia waja Wake wenye kumcha, kuepuka makosa na kuusafisha moyo wake, yanapendeza katika dini na yenye kuteuliwa katika Shari´ah.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Maneno haya yana mambo mawili:

1 – Inafaa kusikiliza melodina toni zenye ladha, kwa sharti ikiwa yule msikilizaji haitakidi jambo la haramu, hasikilizi kitu kilichosimangwa na dini wala hakutumbukia katika matamanio yaliyokatazwa wala pumbao.

2 – Yale yanayomfanya msikilizaji kuingiwa na shauku ya utiifu, kuepuka madhambi, kukumbuka ahadi ya haki na kuutengeneza moyo wake, yanakuwa yenye kupendeza.

Wale ambao wanaona mambo hayo yanapendeza wamejengea hoja zao juu ya nukta hizo mbili. Nukta zote mbili ni za makosa na zimebeba dalili za kijumla. Kwa ajili hiyo nukta mbili hizi zinazochanganya haki na batili, zina maoni ambayo hayakubebwa na yeyote katika wale waliotangulia katika Ummah wala maimamu wake… al-Hasan bin ´Abdil-´Aziyz amesimulia kuwa amemsikia ash-Shaafi´iy akisema:

“Baghdaad nimeacha kitu kilichozuliwa na mazanadiki. Wanakiita Taghbiyr. Kwacho wanawafukuza watu mbali na Qur-aan.”

Taghbiyr ni aina fulani ya midundo yenye kuambatana na uimbaji wa sauti. Hapa tutazungumzia nukta hizi mbili kwa njia inayoendana. Maneno yake:

“Ikijuzu kuyasikiliza pasi namelodi, basi kilicho dhahiri ni kwamba hukumu haibadiliki kwa kuyasikiliza kwa melodi.”

Hoja hii ni mbovu sana. Udhahiri ni kinyume na hivyo. Kule kusema tu kuwa melodiinafaa ni maoni yenye makinzano, kwa sababu waislamu wengi wanaona kinyume na hivyo. Kwa sababu tu melodiyenyewe inafaa, haina maana kwamba sauti ambayo haikuandamana inafaa isipokuwa mpaka kuwepo na dalili inayothibitisha kinyume chake. Nyimbo unaombatana unahitaji hukumu maalum. Pengine mtu akasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisoma Qur-aan, akamuomba Ibn Mas´uud kusoma na akasema wakati wa kisomo cha Abu Muusa:

“Hakika umepewa sauti nzuri ya Daawuud.”[1]

Ambaye atasema kuwa ikiwa yote haya yamefaa pasi na melodi, hukumu inabaki vilevile kwa melodi, amezungumza kidhambi na kwa uwongo kwa maafikiano ya watu wote.

Kuhusu nukta yake ya pili, uchambuzi huo unaanzia kwamba Allaah (Subhaanah) anapenda yale yanayomtia mtu shauku ya kila alichoamrishana kumkumbusha yale aliyowaandalia waja Wake wenye kumcha na kumtahadharisha kutokamana na makosa. Allaah (Subhaanah) anapenda kuwa na shauku kwa yale aliyoyaamrisha na kutahadhari kutokamana na yale aliyoyakataza, anapenda mtu aamini ahadi na matishio Yake na yale yote yanayopelekea katika kumuogopa, kumtaraji, kumpenda na kurejea kwa kutubia Kwake. Aidha anawapenda wale wanaompenda. Anapenda imani, ni mamoja misingi na tanzu zake, anawapenda waumini na kusikiliza kunakopelekea katika yale yanayopendwa. Yale yanayopelekea katika yale yanayopendwa nayo ni yenye kupendwa. Kwa hiyo usikilizaji ni wenye kupendwa.

Nukta hii imejengeka juu ya misingi miwili:

1 – Kuyatambua yale yanayopendwa na Allaah.

2 – Kusikiliza kunapelekea yale yanayopendwa na Allaah, ima kikamilifu au kwa njia yenye nguvu.

Ikiwa usikilizaji unapelekea katika yale anayoyapenda na yale anayoyachukia na yale yanayochukiwa yakawa ndio yenye nguvu zaidi, basi usikilizaji utakuwa wenye kusimangwa. Ikiwa yanalingana yale yanayopendwa na yanayochukiwa, hayatokuwa yenye kupendeza wala yenye kuchukiwa.

Kuhusu msingi wa kwanza, ambao unahusiana na kuyatambua yale yanayopendwa na Allaah, ni jambo rahisi ingawa kuna jopo kubwa la watu wamekosea katika jambo hili.

Kuhusu msingi wa pili, hapo ndipo kunatakiwa kuwekewa mazingatio. Hapo ndipo wamekosea na kupotea waliopotea. Nitalizungumzia hilo kwa njia nyingi na kubainisha lengo:

1 – Ni lazima kutambua kuwa yote yanayohusiana na ´ibaadah, utiifu na dini na mapendekezo, yanatakiwa kurejeshwa katika Shari´ah. Hakuna yeyote mwenye ruhusa ya kuzusha ´ibaadah pasi na idhini ya Allaah na kusema ni kitu kinachopendeza kwa Allaah. Dini na Shari´ah ya Allaah imebadilishwa kwa njia hiyo na kukazuliwa shirki na yale ambayo Allaah hakuyateremshia dalili. Kila kilichotajwa ndani ya Qur-aan, Sunnah na maneno ya Salafna maimamu na Mashaykh wa dini katika kuhamasisha kufuata yale tuliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wetu na njia Yake ilionyooka na makatazo ya yaliyo kinyume nayo – yote hayo yanakataza jambo la kuzusha ´ibaadah ambayo haikuidhinishwa na Allaah, ni mamoja ´ibaadah hiyo anafanyiwa mwingine asiyekuwa Allaah au anafanyiwa Allaah pekee kwa njia ambayo hakuiamrisha. Bali dini ya haki ni kumwabudia Allaah pekee asiyekuwa na mshirika kwa ile njia iliyofikishwa na Mtume Wake… Huu ni msingi mkuu katika njia ya Allaah ambayo inatakiwa kuitendea kazi. Kwa sababu matendo mengi katika Shari´ah ima yanaweza kuwa yenye kuruhusiwa, yenye kuchukiza au ambayo kuna makinzano katika kuruhusiwa au kuchukiza kwake. Pengine vilevile yakawa ya haramu au kuna makinzano katika uharamu wake. Matokeo yake baadhi ya watu wakayapendezesha, kwa sababu wanayaona kuwa ni mazuri na yenye kupendeza mpaka wakafikia kumzingatia yule mwenye kuyafanya ni bora kuliko ambaye hayafanyi. Pengine wakayafanya ni miongoni mwa mambo ya lazima katika kumfikia Allaah au ni moja ya nembo za waja wema na mawalii wa Allaah. Ukweli wa mambo ni kuwa hilo ni kosa, upotofu na kuzusha dini ambayo haina dalili kutoka kwa Allaah. Mfano wa hilo ni unyoaji kipara katika isiyokuwa hajj na ´umrah pasi na udhuru. Ndani ya Qur-aan Allaah ametaja kunyoa na kukata nywele wakati mtu anapokuwa katika hajjna Akataja unyoaji kutokana na udhuru.  Mbali na hali hizo wanazuoni wametofautiana juu ya maoni mawili yanayotambulika kama ni jambo linaloruhusiwa au lenye kuchukiza. Hata hivyo wanazuoni wa waislamu na maimamu wa dini hawakutofautiana kuwa kitendo hicho hakikuwekwa katika Shari´ah na wala hakipendezi, wala sio katika njia ya Allaah na kuipa nyongo kunakokubaliwa na Shari´ah wala si jambo ambalo Allaah amemsifia yeyote katika wale mafukara.Pamoja na hayo, wako baadhi ya wafanya ´ibaadah mafukara na Suufiyyah wamefanya kitendo hicho cha kunyoa kipara ni jambo la kidini tena bora. Wamefikia mpaka kumdharua na kumsema vibaya ambaye hanyoi kipara, na ambaye ananyoa kipara anakuwa katika mwongozo wao. Fikira hii ni upotofu kutokana na njia ya Allaah na ni kuiibadilisha dini kwa makubaliano ya waislamu.

2 – Nyimbo inafanya kupata mapenzi ya Allaah na yale yanayopelekea katika mapenzi ya Allaah yanapendeza kwa Allaah, ni maneno ya batili. Wengi katika watu hawa, kama si wote, wamepotea na kukosea kutokana na taswira hiyo. Wakadhani kuwa nyimbo zinafanya kupata mapenzi ya Allaah. Kwani mapenzi ndio msingi wa imanina kitendo cha moyo na inakamilika kwa kukamilika kwake… Mapenzi na harakati hizi zinazotokana na nyimbo zilizozuliwa na mfano wake sio katika mapenzi yanayopendeza kwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bali zimekusanya yale yasiyopendwa na Allaah na yale yanayomkasirisha Allaah ni mengi zaidi kuliko yale yenye kumpendeza na yasiyomkasirisha. Kuufunganisha moyo na yale yanayopendeza kwa Allaah na kuyakataza ni muhimu zaidi kuliko kuuamsha peke yake. Hata kama jambo hilo linaamsha mapenzi na harakati kwa kudhani kuwa hilo linapendeza kwa Allaah, hilo si jengine isipokuwa ni dhana tu na yale yanayotamaniwa na nafsi. Lakini tayari wameshajiliwa na mwongozo kutoka kwa Mola wao.”[2]

Kwa kifupi ni kwamba, haitoshi kwa sababu tu mifumo ya kisasa inanufaisha eti ndio iwe inakubalika kwa mujibu wa Shari´ah. Kwa sababutumefungamanishwa kwaQur-aan na Sunnah, na si kwa matamanio na kuonja. Kila njia iliyozuliwa, kama mfano wa maigizo na nyimbo,inautikisa moyo, kuufanya moyo kuingiwa na shauku, kuwaamsha waliolala na kuwaongoza njia baadhi ya waliopotea, haina kheri yoyote. Kwa sababu yangelikuwa na kheri, basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliyaweka katika Shari´ah nayangewaongoza kwanza wale wa awali waliotangulia. Yule mtu ambaye anakumbusha na kuongozwa na mfumo kama huo ni haraka sana kumuona anarudi katika hali yake ya zamani. Na endapo atashikamana nayo, basi anaifanya kinyume na njia ilionyooka.

[1] al-Bukhaariy (5048) na Muslim (793).

[2] al-Istiqaamah (1/234-261).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 75-80
  • Imechapishwa: 28/05/2023