Swali 53: Ni vita vipi vilivyotokea mwaka huo?

Jibu: Katika Jamaadaa al-Uulaa kulifanyika vita dhidi ya Banuu Lihyaan, vinavyotambulika pia kama vita vya ´Asafaan. Hapo ndipo swalah ya khofu iliwekwa katika Shari´ah wakati wa ´Aswr.

Mwaka huohuo ndio kulitokea vita vya Dhuu Qarad. Kuna maoni mengine pia yanayosema kuwa vilitokea katika mwaka wa saba. Vilianza wakati ambapo ‘Uyaynah aliwavamia ngamia wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ambapo Salamah bin al-Akwa’ akawarudisha kabla ya wapanda farasi wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwahi kuwafikia. Kwa hiyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimpatia fungu husika la ngawira za kivita za mpanda farasi na askari wa kutembea kwa miguu.

Katika Sha´baan ikawa vita dhidi ya Banuul-Mustwaliq. Juwayriyyah, mke wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akatekwa na yeye ndio akawa sababu ya kuachiliwa mateka yao. Katika vita hivyo hivyo ndio Ibn Abiy Saluul aliwazungumza vibaya Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo kukashushwa juu yake Suurah ”al-Munaafiquun”.

Mwaka huohuo ndio kulitokea uwongo. Kukateremshwa Aayah kumi na tano ndani ya Suurah ”an-Nuur” zinazomtakasa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa). Wale waliomchafua wakasimamishiwa adhabu.

Baadhi yao wanazingatia tukio la Hudaybiyah kuwa ni vita kutokana na lilivyoishilia na kiapo kilicholiwa hapo. Wengine hawazingatii hivo kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakutoka kwenda huko kwa lengo la kupigana.

  • Mhusika: ´Allaamah Haafidhw bin Ahmad al-Hakamiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Amaaliy fiys-Siyrah an-Nabawiyyah, uk. 116-117
  • Imechapishwa: 19/10/2023