52. Dalili inayofahamisha uola wa Allaah na kustahiki Kwake kuabudiwa IX

Amesema (Ta´ala):

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi. Anafunika usiku kwa mchana, unaufuatia upesiupesi na [ameumba] jua na mwezi na nyota vimetiishwa kwa amri Yake.”[1]

Kulingana Kwake juu ya ´Arshi kumetokea baada ya kuumba mbingu na ardhi. Kwa sababu ni miongoni mwa sifa Zake za kimatendo ambazo Allaah anazifanya pale anapotaka.

Maana ya kulingana ni kuwa juu.

´Arshi ndio paa la viumbe.

Maana ya ´Arshi kilugha ni kiti. Ni kiti kilicho na miguu kinachobebwa na Malaika. ´Arshi ndio kiumbe kikubwa na kilicho juu zaidi.

Kulingana ni sifa miongoni mwa sifa za Allaah za kimatendo kama inavyolingana na utukufu Wake. Sio kama kulingana kwa viumbe juu ya viumbe. Wala Yeye hana haja ya ´Arshi. Yeye ndiye ambaye anaizuia ´Arshi na vyenginevyo:

إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا ۚ وَلَئِن زَالَتَا إِنْ أَمْسَكَهُمَا مِنْ أَحَدٍ مِّن بَعْدِهِ

“Hakika Allaah anazuia mbingu na ardhi zisiondoke na zikiondoka basi hakuna yeyote wa kuzishikilia baada Yake.”[2]

´Arshi ni yenye kumuhitajia Allaah (´Azza wa Jall) kwa sababu imeumbwa. Allaah ni mkwasi juu ya ´Arshi na vyenginevo. Lakini amelingana juu Yake kwa hekima anayoijua Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kulingana ni aina fulani ya ujuu. Lakini ujuu ni sifa ya kidhati. Lakini kulingana ni sifa ya kimatendo anaiyofanya anapotaka (Subhaanahu wa Ta´ala).

يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ

”Anafunika usiku kwa mchana… “

Anaufunika usiku kwa mchana na anaufunika mchana kwa usiku. Pindi mnapoona ulimwengu unangaa tahamaki unafunikwa na usiku na unakuwa wenye giza na usiku unafunikwa na mchana na tahamaki unakuwa wenye kuangaza:

يَطْلُبُهُ حَثِيثًا

”… unaufuatia upesiupesi.”

Hiki kinakuja moja kwa moja baada ya hiki na hakichelewi. Unapoingia usiku unakuja mchana na unapoingia mchana unakuja usiku papo kwa hapo na kimoja hakichelewi kutokamana na kingine. Haya ni katika ukamilifu wa uwezo Wake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Jua ni nyota kubwa inayojulikana. Vivyo hivyo kuhusu mwezi ni nyota miongoni mwa zile sayari saba kubwa. Kila kimoja katika viwili hivyo kinatembea na kuizunguka ardhi. Ardhi imetulia na iko imara. Allaah ameifanya kuwa yenye kuthibiti kwa ajili ya manufaa ya waja. Jua na sayari zengine zinazunguka juu yake. Mambo si kama wanavosema wahitimu wa leo wanaodai elimu kwamba jua ndio limetulia na ardhi ndio inalizunguka. Haya ni kinyume na yaliyotajwa ndani ya Qur-aan:

وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا

“Na jua linatembea hadi matulio yake.”[3]

Wao wanasema kuwa jua limetulia. Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu!

Nyota ni sayari ambazo zimedhalilishwa kwa amri Yake. Zimedhalilishwa katika kutembea na kuzunguka kwake siku zote. Hapa kuna Radd juu ya wale wanaoabudu jua, mwezi na nyota kwamba vimedhalilishwa kwa amri ya Allaah na ni vyenye kuamrishwa. Allaah ndiye anayevifanya kutembea. Allaah ndiye anayevisimamisha anapotaka (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa hiyo ni vyenye kuendeshwa na havina maamuzi yoyote. Allaah (Subhaanah) anaviamrisha, kuviendesha na vinaangaza kwa amri Yake ya kilimwengu. Kinachomoza kimoja, kinazama kingine na vinapishana.

[1] 07:54

[2] 35:41

[3] 36:38

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 113-116
  • Imechapishwa: 21/12/2020