51. Dalili inayofahamisha uola wa Allaah na kustahiki Kwake kuabudiwa III

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Vilevile amesema (Ta´ala):

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ يَطْلُبُهُ حَثِيثًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومَ مُسَخَّرَاتٍ بِأَمْرِهِ ۗ أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi. Anafunika usiku kwa mchana, unaufuatia upesiupesi na [ameumba] jua na mwezi na nyota vimetiishwa kwa amri Yake. Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.”[1]

MAELEZO

Mola wenu – Bi maana Muumbaji wenu na anayekuleeni kwa neema Zake.

Ni Allaah – Bi maana hakuna mwengine asiyekuwa Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Kisha akataja dalili ya hayo kwa kusema:

 الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ

”Ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita.”

Hii ndio dalili ya uola wa Allaah (´Azza wa Jall). Kwamba Yeye ameumba mbingu na ardhi na hakuna yeyote aliyeumba chochote katika hayo. Hakuna yeyote aliyemsaidia (Subhaanahu wa Ta´ala) katika hayo. Bali Yeye amepwekeka katika hayo:

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ

”Ameumba mbingu na ardhi… ”

Kuna yeyote katika washirikina au wakanamungu ambaye amepingana na haya na akasema kuwa sio Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi na kwamba ameviumba ni fulani, yeye ndiye kaviumba au sanamu fulani ndiye kaviumba? Je, kuna yeyote katika walimwengu aliyeyasema haya hapo zamani mpaka hii leo licha ya kuwa Aayah hii inasomwa usiku na mchana? Hakuna yeyote aliyepingana na hilo na wala hawezi kupingana nayo kabisa.

فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ

”… katika siku sita.”

Uumbaji huu mkuu na mkubwa Allaah amewaumba katika siku sita. Yeye ni muweza wa kuwaumba mara moja. Lakini amewaumba kwa muda wa siku sita kwa hekima anayoijua Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Siku sita hizi ya kwanza yake ni siku ya jumapili na ya mwisho yake ni siku ya ijumaa. Siku ya ijumaa ndio uumbaji ulikamilika. Kwa ajili hiyo ndio maana siku hii ikawa ni siku tukufu zaidi ya wiki. Siku hiyo ndio bwana ya masiku, sikukuu ya wiki na ndio siku bora zaidi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema.

“Siku bora iliyochomozewa na jua ni siku ya ijumaa.”[2]

Kwa sababu siku hiyo ndio kulikamilika uumbaji wa viumbe. Siku hiyo ndio ameumbwa Aadam, siku hiyo ndio kaingia Peponi na siku hiyo ndio akashuka kutoka ndani yake. Siku ya ijumaa ndio Qiyaamah kitasimama. Yote hayo siku ya ijumaa. Ndio siku bora. Ndio siku ya mwisho ya uumbaji wa mbingu, ardhi na vilivyomo ndani yavyo.

[1] 07:54

[2] Muslim (854), Abu Daawuud (1046), at-Tirmidhiy (488) na an-Nasaa´iy (03/90).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 111-113
  • Imechapishwa: 21/12/2020