45. Chukula walichozowea kula waarabu

262 – ´Abdur-Rahmaan bin Waaqid ametuhadithia: Dhwamrah ametuhadithia, kutoka kwa ´Uthmaan bin ´Atwaa’, kutoka kwa baba yake, ambaye amesema:

”Abu Hurayrah aliwaona watu Palestina waliomletea mikate ya bapa iliyookwa, ambapo akaanza kulia. Akaambiwa: ”Ee Abu Hurayrah! Ni kipi kinachokuliza?” Akajibu: ”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwahi kuyaona haya kwa macho yake mpaka alipoacha dunia.”

263 – Muhammad bin ´Amr al-Baahiliy ametuhadithia: Mu´aadh bin Hishaam amenihadithia: Baba yangu amenihadithia, kutoka kwa Yuunus, kutoka kwa Qataadah, kutoka kwa Anas bin Maalik, ambaye amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwahi kula kwenye meza ya chakula wala au kutoka kwenye sahani ya chakula cha kumalizia. Wala hakutengenezewa mkate wa bapa.” Nikasema: ”Walikuwa wanakula kwenye kitu gani?” Akasema: ”Juu ya sakafu.”[1]

264 – Muhammad bin Idriys ametuhadithia: Zuhayr bin ´Abbaad ametuhadithia: ´Atwaa’ bin Muslim ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash: Sa´iyd bin Jubayr alinambia:

”Siku moja nilimtengenezea Ibn ´Abbaas na wenzake aina mbalimbali ya vyakula na Khabisw[2], ambapo akanambia: ”Ee Sa´iyd, sisi ni waarabu! Tufanyie badala yake uji na Hays[3]. Usingelikuwa ni mmoja katika sisi, basi nisingeyakwambia haya.”

265 – Ibraahiym bin Sa´iyd amenihadithia: ar-Rabiy´ bin Naafiy´ ametuhadithia: Ismaa´iyl bin ´Ayyaash ametuhadithia, kutoka kwa Shurahbiyl bin Muslim, aliyesema:

”´Uthmaan bin ´Affaan alikuwa akiwatengenezea watu chakula cha wakuu, ambapo anaingia nyumbani kwake akila siki na mafuta.”

266 – Ibraahiym bin Sa´iyd al-Jawhariy amenihadithia: Husayn bin Muhammad ametuhadithia: Sulaymaan bin Qarm ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Shaqiyq, ambaye amesema:

”Mimi na rafiki yangu mmoja tuliingia kwa Salmaan. Akatukaribisha mkate na chumvi kisha akasema: ”Lau Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakutukataza kuchupa mipaka, basi nisingelichupa mipaka kwa ajili yenu.” Rafiki yangu akasema: ”Unasemaje kama kwenye chumvi yetu kungelikuwa na thyme?” Akatuma bakuli kwa mfanyabiashara wa manukato, akaifunga, kisha akamletea thyme.”

267 – al-Mufadhdhwal bin Ghassaan ametuhadithia, kutoka kwa al-Aswma´iy, kutoka kwa Ishaaq bin Ibraahiym, ambaye amesema:

”Niliingia kwa Kahmas al-´Aabid, akatuletea tende kumi na moja ambazo hazijaiva na kusema: ”Hiki ndio chote alinachonacho ndugu yenu. Allaah ndiye Mwenye kutakwa msaada.”

268 – al-Qaasim bin Zakariyyaa bin Diynaar ametuhadithia: Ishaaq ametuhadithia, kutoka kwa Mansuur, kutoka kwa Mundhir, kutoka kwa Yuunus, kutoka kwa al-Qaasim, aliyesema:

”´Aaishah alinitumia dirhamu mia akasema: ”Waalike watu chakula juu ya tohara ya mtoto ya wako wa kiume.”

269 – al-Qaasim ametuhadithia: Ishaaq bin Mansuur ametuhadithia, kutoka kwa Qays, kutoka kwa Jaabir, kutoka kwa al-Qaasim, aliyesema:

”Bwana mmoja alitoa dirhamu moja wakati wa tohara ya mtoto, ambapo Shurayh akasema: ”Ngamia na kingine kinachofaa. Pesa zilizobaki zinatakiwa kuhifadhiwa.”

[1] at-Tirmidhiy (1788), aliyesema Hadiyth ni nzuri na geni, na Ibn Maajah (3292).

[2] Tamtam iliyotengenezwa kwa tende na siagi. 

[3] Mchanganyiko wa unga ulio na tende, jibini na siagi.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 157-162
  • Imechapishwa: 02/08/2023