46. Unapoalikwa chakula nyumbani kwa watu

270 – Fadhwl bin Ishaaq amenihadithia: Abu Usaamah ametuhadithia, kutoka kwa Sulaymaan bin al-Mughiyrah, kutoka kwa Thaabit, ambaye amesema:

”´Umar bin al-Khattwaab alitamani kinywaji, ambapo akaletewa kinywaji cha asali. Akawa anageuza kikombe mkononi mwake na kusema: ”Nikikinywa, utaondoka utamu wake na kubaki matokeo yake.” Kisha akampa nacho mtu mwingine.”

271 – Muhammad bin Abiy Samiynah ametuhadithia: Muhammad bin ´Abdillaah al-Answaariy ametuhadithia: Abaan bin Swam´ah ametuhadithia, kutoka kwa Bakr bin ´Abdillaah, aliyesema kuhusu:

ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ

”Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema!”[1]

”Ataulizwa. Atafanyiwa hesabu mpaka ya kile kinywaji alichokunywa kwenye nyumba ya watu.”

272 – Shujaa´ bin al-Ashras ametuhadithia: Hashraj bin Nabaatah ametuhadithia, kutoka kwa Abu Naswr, kutoka kwa Abu ´Asiyb, aliyesema:

”Usiku mmoja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka nje na kunipitia. Akaniita na nikatoka kumwendea. Akampitia Abu Bakr na kumwita, ambapo akatoka kumwendea. Kisha akampitia ´Umar na kumwita, ambapo akatoka kumwendea. Akaendelea mpaka alipoingia kwenye shamba ya baadhi ya Answaar. Akamwambia mwenye shamba: ”Tupe tende ambazo hazijaiva za tule.” Bwana yule akaleta rundo na kuliweka chini. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake wakala. Kisha akaagiza maji ya baridi akanywa. Halafu akasema: ”Hakika mtaulizwa juu ya neema hii siku ya Qiyaamah.” ´Umar akachukua rundo lile na kulipiga ardhini, ambapo tende zile ambazo zilikuwa hazijaiva zikatawanyika huku na kule. Kukasemwa: ”Ee Mtume wa Allaah, kweli tutaulizwa juu ya haya siku ya Qiyaamah?” Akasema: ”Ndio, isipokuwa tu mambo matatu: kitambaa kinachofunika uchi wako, kipande cha mkate kinachoshibisha njaa yako na nyumba inayokulinda kutokana na baridi na joto.”[2]

273 – Zakariyyaa bin al-Haarith bin Maymuun al-´Abdiy ametuhadithia: Wahb bin Jariyr ametuhadithia, kutoka kwa baba yake: Nimemsikia Muhammad bin al-Munkadir akisimulia kutoka kwa Jaabir bin ´Abdillaah, ambaye amesema:

”Siku moja tuliingia kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh). Akaagiza chakula, lakini hakikuwepo. Akaamrisha kondoo. Tukakamuliwa maziwa na kukapikwa, ambapo sisi na yeye akala. Kisha akaswali na hakutawadha.”

274 – ´Aliy bin Ibraahiym al-Yashkuriy ametuhadithia: Ya´quub bin Muhammad az-Zuhriy ametuhadithia: ´Abdul-Muhaymin bin ´Abbaas ametuhadithia: Abu Haazim ametuhadithia:

”Baada ya ´Aswr niliondoka kwenda kwa Sahl bin Sa´d, alikuwa amefunga.” Ilipofika jioni nilisema kumwambia kijana wake: ”Lete futari yake.” Akasema: ”[Tupu].” Ndipo nikasema: ”Tende nazo?” Akasema: ”Hakuna hata tende.” Nikaanza kumtukana na kusema: ”Umempoteza mzee kutoka katika Maswahabah wake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Akasema: ”Kosa langu ni lipi? Leo amefungua ghala yake na hakuacha nafaka yoyote isipokuwa aliigawanya.”

[1] 102:8

[2] Ahmad (5/81).

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 162-165
  • Imechapishwa: 02/08/2023