Wala tafsiri hii haipingani na Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh):

”Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipojichagulia juu ya nafsi yake Swafiyyah bint Hayayy kati ya mateka ya Khaybar, Maswahabah wakasema: ”Hatujui atamuoa au atamfanya tu kuwa kijakazi wake. Akimsitiri basi atakuwa ni mke wake na asipomsitiri atakuwa ni kijakazi wake.” Wakati ilipofika wakati wa kupanda kipando (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamfunika mpaka akaketi juu ya mgongo wa ngamia. Ndipo wakajua kuwa amemuoa[1].”[2]

Hakuna mgongano wowote kati ya Hadiyth hii na ile tafsiri niliyochagua ya Aayah. Kwa sababu Hadiyth haipingi jilbaab, isipokuwa kinachopingwa ni kujisitiri. Kupinga kujisitiri hakupelekei kupinga jilbaab kabisa. Kuna uwezekano vilevile kukanusha kunakusudia jilbaab ambayo inajumuisha kufunika uso pia, kama ilivyotajwa kwa uwazi katika ule upokezi mwingine:

”Akaweka shuka yake juu ya mgongo na uso wake… ”

Nadharia hii itatiliwa nguvu na yale yanayokuja mbele. Kwa sifa hii ya kipekee ndio ambayo iliwafanya Maswahabaha kuweza kuwatofautisha kati ya wakeze (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) na wajakazi wake. Hiyo ndio maana ya maneno yao:

”Akimsitiri basi atakuwa ni mke wake na asipomsitiri atakuwa ni kijakazi wake.”

Bi maana asipomsitiri usoni mwake. Haina maana ya kuacha wazi sehemu nyingine ya mwili ya kijakazi. Kwa njia hiyo Hadiyth imeafikiana na Aayah[3].

[1] Imekuja katika upokezi mwingine:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) akamfunika na akambeba kwa nyuma yake. Akaweka shuka yake juu ya mgongo na uso wake kisha  akaifunga chini ya miguu yake. Akapanda naye na kumfanya sawa na wake zake wengine.”

[2] al-Bukhaariy, Muslim, Ahmad na Ibn Sa´d na upokezi mwingine ni wake. Ibn-ul-Qayyim  ameegemea juu yake katika “Zaad-ul-Ma´aad”.  Hadiyth imepokelewa pia na al-Bayhaqiy.

[3] Maneno ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah juu ya suala hili ni ya ajabu. Amesema:

”Sitara ni jambo linawahusu wanawake waungwana na si wajakazi. Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah zake ilikuwa wanawake waungwana wanajisitiri na wajakazi wanajiacha wazi.” (Tafsiyr Suurat-in-Nuur, uk. 56)

Inashangaza kuona ananasibisha mwenendo huo katika zama za Mtume (Swalla Alalahu ´alayhi wa sallam). Kwa maana nyingine Mtume (Swalla Alalahu ´alayhi wa sallam) aliyakubali. Endapo kungelikuwa na dalili sahihi na ya wazi juu ya suala hilo basi ingelikuwa ni hoja yenye kutosha kudai kuwa wanawake wa kiumini peke yao ndio wanaotakiwa kujisitiri na kwangu kujirejea kutokamana na maoni yangu. Lakini mimi sioni upokezi hata mmoja, sembuse kusihi. Kubwa liliopo juu ya suala hilo ni Hadiyth ya Anas – na Ibn Taymiyyah hakuleta zaidi ya hiyo – na umekwishajua yaliyomo katika Hadiyth ya Anas – na Allaah ndiye mjuzi zaidi. Sikupenda kuingia kwa undani kuzungumzia hijaab ya mwanamke kwa sababu si mada yetu hii leo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 94-96
  • Imechapishwa: 24/09/2023