41. Hakuna tofauti kati ya kijakazi na mwanamke muungwana

Ibn Hazm ametamka maneno mazuri pale aliposema:

”Ama kutofautisha kati ya mwanamke muungwana na kijakazi, dini ya Allaah ni moja, maumbile na tabia ni moja. Yote hayo yanahusu wanawake wa kiungwana na wajakazi mpaka kuje dalili inayotofautisha kati yao.”

Kisha akasema:

”Baadhi wanajengea hoja kwa maneno Yake Allaah (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاء الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ذَلِكَ أَدْنَى أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

“Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako – na wanawake wa waumini – wajiteremshie Jilbaab zao; hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”

ili kufikia kwamba Allaah (Ta´ala) amewaamrisha kufanya hivo kwa sababu mafusaki walikuwa wakiwasumbua wanawake wa kiumini. Matokeo yake ndipo Allaah akawaamrisha kuvaa jilbaab ili watenda madhambi watambue kuwa ni wanawake waungwana na hivyo wasiwasumbue[1].

Sisi tunajilinda kwa Allaah kutokana na tafsiri hii mbovu ambayo ima inatokana na kuteleza kwa mwanachuoni au unyonge wa mtu mwenye busara au uzushi wa mwongo na mtenda dhambi. Kwa mujibu wa tafsiri hii ni kwamba Allaah amewapa ruhusa watenda maasi kuwasumbua wajakazi wa Kiislamu. Hili ni janga. Hakuna muislamu yeyote mwenye kuonelea tofauti juu ya kwamba imeharamishwa kuzini na wajakazi kama ilivyoharamishwa kuzini na wanawake waungwana na kwamba adhabu anayopewa mwanamke muungwana aliyezini ndio adhabu anayopewa mwanamke wa kijakazi aliyezini. Hakuna tofauti katika jambo hilo. Kuwanyanyasa wanawake wajakazi ni khatari kama ilivyo kuwanyanyasa wanawake waungwana. Kwa ajili hiyo haifai kuyakubali maneno ya yeyote, mbali na ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), isipokuwa yakiwa na cheni yenye kuungana mpaka kwake (´alayhis-Salaam).”[2]

[1] Kwa mujibu wa maoni haya ni kuwa mwanamke hahitajii kuvaa jilbaab ikiwa hakuna watenda madhambi au wakati ambapo hakuna wajakazi, kwa kuwa sababu itakuwa imeondoka. Na inapoondoka sababu inaondoka vilevile hukumu iliyojengeka juu ya sababu hiyo. Kuna mmoja katika waandishi wa leo ameyatamka haya waziwazi na akasema:

”Tanabahini kuwa mapokezi hayo yanahusiana na Aayah katika ”al-Ahzaab”. Kwa sababu mavazi ya wanawake waungwana na wajakazi yalikuwa yenye kufanana. Watenda maasi walikuwa wakiwasumbua wanawake pasi na kupambanua. Ndipo kukateremshwa Aayah ili kupambanua mavazi ya wanawake wa kiungwana ili watambulike na hivyo wasinyanyaswe. Kwa msemo mwingine udharurah ulikuwa katika kipindi hicho peke yake.”  (al-Qur-aan wal-Mar’ah, uk. 59)

Ni kana kwamba anataka kusema kwamba hii leo hakuna udharurah wa jilbaab kwa sababu wanawake wote ni waungwana. Tazama namna ambavyo ujinga wa baadhi ya mapokezi unapelekea kuibatilisha amri ya Qur-aan na Sunnah!

[2] al-Muhallaa (3/218-219). Anaashiria maneno ya ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo alitofautisha kati ya mwanamke muungwana na kijakazi inapokuja katika suala ka kuvaa shungi. az-Zayla´iy ameitaja katika ”Naswb-ur-Raayah” (1/300) na akasema:

”Mapokezi kutoka kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) juu ya jambo hilo ni Swahiyh.”

Upokezi kama huo umepokelewa na Ibn Abiy Shaybah na al-Bayhaqiy. Ibn Hazm ameandika kwamba alikuwa ni mwenye kuyatambua na akasema:

”Lakini hakuna maneno, mbali na ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), yanayotumiwa kama hoja.” (al-Muhallaa (3/221))

Yanatiliwa nguvu na maneno ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa):

”Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoingia kwake akajificha kijakazi wao. Akauliza: ”Amepata hedhi?” Wakasema: ”Ndio.” Akapasua kilemba chake pande mbili na kusema: ”Jifunike kwa hiki.”

Ameipokea Ibn Abiy Shaybah na Ibn Maajah kwa cheni ya wapokezi dhaifu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 92-94
  • Imechapishwa: 24/09/2023