Kwa vile tumetaja njia mbili mpya za ulinganiziambazo zilikemewa na Salaf hapo kale, tutataja mambo mawili mepya yaliyozuliwa hii leo katika njia za kulingania ambazo zimekemewa na wanazuoni wa Ahl-us-Sunnah Salafiyyah kutokana na uzushi wao na kutoka nje ya mfumo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

1 – Uigizaji. Wajinga, au wapotofu, wameifanya kuwa ni njia miongoni mwa njia za kulingania kwa Allaah (Ta´ala). Wanazuoni wengi wameandika na kukemea uigizaji na wakatoa fataawaa zinazoharamisha na kubatilisha kitu hicho. Kwa sababu uigizaji ni mfumo uliozuliwa ndani ya Shari´ah ya Allaah (Ta´ala) kwa kuwa ni miongoni mwa mambo yaliyozuliwa ndani ya dini. Miongoni mwa hayo ni maneno ya Shaykh Hamuud bin ´Abdillaah at-Tuwayjiriy (Rahimahu Allaah):

“Kuigiza wakati wa kulingania kwa Allaah (Ta´ala) sio katika Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Sunnah za makhaliyfah wake waongofu na walioongozwa. Uigizaji ni miongoni mwa mambo yaliyozuliwa katika zama zetu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha mambo yaliyozuliwa na akaeleza kurudishwa kwake nyuma na akaeleza kuwa ni maovu na upotofu:

“Ninakuusieni kumcha Allaahna kusikiliza na kutii hata kama mtataliwa na mtumwa. Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu. Shikamaneni nazo kwelikweli na ziumeni kwa magego. Tahadharini na mambo yenye kuzuliwa, kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[1]

Hadiyth hii ndio msingi mkuu wa kukataza filamu na kuingizwa kwake katika kulingania kwa Allaah (Ta´ala), kwa sababu hazikuwa ni katika Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala za makhaliyfah wake waongofu.

Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa na kila Bid´ah ni upotevu.”[2]

Imekuja kwa an-Nasaa´iy:

“Hakika mazungumzo ya kweli kabisa ni Kitabu cha Allaah na uongofu mzuri kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa, kila kilichozuliwa ni Bid´ah, kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”[3]

Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

Hadiyth hii ni msingi mkuu unaokataza uigizaji na kuingizwa kwake katika njia za kulingania kwa Allaah (Ta´ala), kwa sababu uigizaji haikuwa ni miongoni mwa mwongozo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – ni miongoni mwa mambo mepya yaliyozuliwa katika karne ya nne baada ya Kuhajiri.

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayezua katika amri yetu hii kile kisichokuwemokitarudishwa.”[4]

Imekuja katika upokezi mwingine:

“Yeyote atakayefanya katika amri yetu hii kisichoafikiana na amri yetu kitarudishwa.”[5]

Hadiyth zote hizi zinasambaratisha zile shubuha ambazo zinatumiwa na watu wanaojuzisha uigizaji.

Yakishatambulika hayo, hakuna yeyote awezaye kudai kuwa uigizaji umefanywa kwa amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba ameamrishwa zifanywe ni njia ya kulingania kwa Allaah (Ta´ala). Ambaye atafanya jeuri na kudai kinyume chake basi atalazimika kuleta dalili ya kinabii juu ya madai yake – kitu ambacho hatoweza.”[6]

[1] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2455).

[2] Muslim (592), Ahmad (3/310) na al-Bayhaqiy (3/313).

[3] Muslim (867), Ibn Maajah na wengineo.

[4] Muslim (1718).

[5] al-Bukhaariy (2697).

[6] Tahdhiyr-ul-´Aaqil an-Nabiyl, uk. 7-10. Shaykh (RahimahuAllaah) kwa kitabu hiki alikuwa anamraddi mtunzi wa kitabu ”Hukm-ut-Tamthiyl fiyd-Da´wah ilaa Allaah”

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 51-53
  • Imechapishwa: 22/05/2023