Tawhiyd ni kitu gani? Je, ni kule mtu kukubali kwamba Allaah ndiye muumbaji, mruzukaji, muhuishaji na mfishaji? Hapana. Tawhiyd ni kule kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah. Kwa sababu Allaah amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[1]

Wanazuoni wa tafsiri ya Qur-aan wamesema:

لِيَعْبُدُونِ

“Waniabudu.”

maana yake wanipwekeshe. Wakaifasiri Tawhiyd kwa ´ibaadah.

Kwa hivyo Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah na sio kukubali kwamba Allaah ndiye muumbaji, mruzukaji, muhuishaji, mfishaji na mwenye kuyaendesha mambo. Kwa sababu jambo hilo tayari lipo katika maumbile na lipo kwenye akili za wenye akili. Hakuna mtu mwenye akili duniani anayeaona kwamba kuna yeyote aliyeumba mbingu na ardhi isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna yeyote ulimwenguni kote na waliyomo katika makafiri na wakanamungu anayeitakidi kwamba kuna yeyote aliyemuumba mtu:

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ

“Ukiwauliza: “Ni nani kawaumba?” Bila shaka watasema: “Allaah.”[2]

Hakuna mwenye akili yoyote ulimwenguni anayeitakidi kuwa kuna mtu ambaye amemuumba mtu anayetembea ardhini, anazungumza, anakula na anakunywa. Hivi kuna mwenye akili anayeamini hivi?

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ  أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ

“Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaji au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini.”[3]

Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah tayari ipo katika maumbile na akili. Lakini haitoshi pasi na Tawhiyd-ul-´Ibaadah ambayo ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah. Ndio maana Shaykh akasema:

“Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah”

Sio kumpwekesha Allaah kwa uumbaji, uruzukaji, uhuishaji na ufishaji. Kwa sababu haya ni mambo yanayotambulika. Jengine ni kwa sababu Tawhiyd-u-Rubuubiyyah haitoshi katika kuiarifisha Tawhiyd.

[1] 51:56

[2] 43:87

[3] 52:35-36

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 81
  • Imechapishwa: 27/12/2020