38. Kubwa ambalo Allaah amewakataza waja ni shirki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kubwa Alilokataza Allaah ni Shirki, nako ni kuomba wengine pamoja Naye.

MAELEZO

Kubwa alilokataza Allaah… – Hii ni faida kubwa. Kwani wapo watu wanaoamini kwamba yapo mambo ambayo ndio maovu makubwa na ndio makubwa ambayo Allaah amekataza na utawasikia wakisema kuwa ribaa na uzinzi ndio haramu zilizo kubwa. Kwa ajili hiyo wanakokoteza kukataza ribaa, uzinzi na uharibifu wa tabia. Lakini sambamba na hilo hawatilii umuhimu jambo la shirki na wala hawaikatazi ilihali wanaona watu wanatumbukia ndani yake. Huu ni mjinga mkubwa juu ya Shari´ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kubwa alilokataza Allaah ni shirki. Ndio jambo kubwa kuliko ribaa, kunywa pombe, wizi, kula mali za watu kwa dhuluma, kamari na mengineyo. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا

”Sema: “Njooni nikusomeeni yale Aliyoyaharamisha Mola wenu kwenu kwamba: “Msimshirikishe na chochote; na muwafanyie wema wazazi wawili.”

Aayah hizi zinaitwa nyasia kumi:

قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ

”Sema: “Njooni nikusomeeni yale Aliyoyaharamisha Mola wenu kwenu.”

Mpaka aliposema:

ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ

“Hivyo ndivyo alivyokuusieni kwayo mpate kuelewa.”[1]

Maharamisho haya Allaah ameyaanza kwa kusema:

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا

“Wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mungu mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah ameiharamisha isipokuwa kwa haki na wala hawazini – na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu.”[2]

Ikafahamisha kwamba shirki ndio jambo kubwa alilokataza Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema katika Suurah “al-Israa´”:

لَّا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتَقْعُدَ مَذْمُومًا مَّخْذُولًا

”Usifanye pamoja na Allaah mungu mwengine, ukaja kusemwa vibaya na mwenye kutupiliwa mbali.”[3]

 Ameanza kwa shirki na akamalizia kwa kukataza shirki pale aliposema:

وَلَا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتُلْقَىٰ فِي جَهَنَّمَ مَلُومًا مَّدْحُورًا

”Na wala usifanye pamoja na Allaah mungu mwengine ukaja kutupwa katika Moto hali ya kuwa mwenye kulaumiwa na kufukuziliwa mbali.”[4]

Ni dalili inayofahamisha kwamba ndio jambo kubwa alilokataza Allaah. Hayo yanajulishwa na maneno ya Shaykh:

“Kubwa alilokataza Allaah ni shirki.”

Imepokelewa katika Hadiyth Swahiyh kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Aliulizwa ni dhambi ipi kubwa zaidi?” Akajibu: “Ni kumfanyia Allaah mshirika ilihali Yeye ndiye kakuumba.” Kisha kukasemwa: “Kisha ipi?” Akajibu: “Kumuua mtoto wako kwa kuchelea kula pamoja nawe.” Kukasemwa: “Kisha ipi?” Akajibu: “Kumzini mke wa rafiki jirani yako.”[5]

Ndipo Allaah akateremsha hali ya kuyasadikisha hayo kwa kusema:

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا

“Wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mungu mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah ameiharamisha isipokuwa kwa haki na wala hawazini – na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu.”

Akaanza kwa shirki. Aliposema:

“Ni kumfanyia Allaah mshirika… “

Bi maana mwenza. Amesema kuwa ndio dhambi kubwa zaidi baada ya kuulizwa ni dhambi ipi kubwa zaidi. Ndipo akaanza kwa shirki. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jiepusheni na madhambi saba yenye kuangamiza.” Kukasemwa: “Ni yepi, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Kumshirikisha Allaah, uchawi, kuiua nafsi ambayo Allaah ameharamisha kuiua isipokuwa kwa haki… “[6]

Akaanza kwa shirki. Ikawa ni dalili inayoonyesha kuwa shirki ndio dhambi kubwa. Kwa ajili hiyo mshirikina hatoingia Peponi. Amesema (Ta´ala):

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah, basi hakika Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni motoni – na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kuwanusuru.”[7]

Allaah hamsamehi mshirikina:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[8]

Ni dalili inayoonyesha kuwa Pepo imeharamishwa kwa mshirikina. Jengine ni kwamba Allaah hamsamehi. Ni dalili iliyofahamisha kwamba shirki ndio dhambi kubwa. Kwa sababu madhambi mengine, mbali na shirki, yanasamehe:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”

Uzinzi, wizi, unywaji pombe na ribaa yote yanaingia ndani ya utashi wa Allaah; Allaah akitaka atamsamehe mwenye nayo na akitaka atamuadhibu.

[1] 06:151-152

[2] 25:68

[3] 17:22

[4] 17:39

[5] al-Bukhaariy (6861) na Muslim (86).

[6] al-Bukhaariy (6866) na Muslim (89).

[7] 05:72

[8] 04:48

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 81-86
  • Imechapishwa: 10/12/2020